Home VIWANDA Kiwanda cha Stalick chaleta maendeleo Pwani

Kiwanda cha Stalick chaleta maendeleo Pwani

0 comments 437 views

Kiwanda cha kuzalisha unga wa chokaa (ground calcium carbonate) cha Stalick, kimeendelea kuwa chachu ya maendeleo kwa jamii inayozunguka eneo hilo kwa kutoa ajira na kuchangia shughuli mbalimbali za kijamii.

Akizungumza kupitia mahojiano maalum, Meneja wa kiwanda hicho kilichopo katika Kata ya Msoga, Wilaya ya Chalinze mkoani Pwani, Expeditor Mlanzi amesema kuwa zaidi ya asilimia 98 ya wafanyakazi wa kiwanda hicho ni vijana kutoka maeneo ya jirani, jambo ambalo limeleta mwamko mpya wa kiuchumi kwa familia na jamii kwa ujumla.

Kiwanda cha kuzalisha unga wa chokaa (ground calcium carbonate) cha Stalick.

Meneja wa kiwanda kuzalisha unga wa chokaa (ground calcium carbonate) cha Stalick kilichopo katika Kata ya Msoga, Wilaya ya Chalinze mkoani Pwani, Expeditor Mlanzi.

“Ajira hizi zimekuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo ya kiuchumi kwa mtu mmoja mmoja na jamii, kwani vijana wengi sasa wanapata kipato cha uhakika kupitia nafasi walizopata katika kiwanda chetu,” amesema Mlanzi.

Mbali na ajira, kiwanda hicho kimekuwa kikitekeleza miradi mbalimbali ya kijamii ikiwa ni sehemu ya uwajibikaji wa kampuni kwa jamii (CSR).

Miongoni mwa miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa darasa na kisima cha maji katika Shule ya Msingi Rubani, pamoja na uboreshaji wa vyoo katika Shule ya Msingi Changa.

Aidha, Mlanzi ameongeza kuwa kiwanda kinanunua malighafi na kufanya shughuli za uchimbaji katika maeneo ya karibu kama Ukerewe, Rubaya, Msolwa na Nkuta hali inayochochea zaidi mzunguko wa fedha na uchumi katika maeneo hayo.

“Tunashirikiana kwa karibu na mamlaka za serikali za mitaa, halmashauri, taasisi kama TANESCO na wadau wengine, hasa katika kushiriki shughuli mbalimbali za kijamii na kitaifa, ikiwemo Mwenge wa Uhuru.

Kwa ujumla, kiwanda cha Stalick kimejipambanua kuwa mdau muhimu wa maendeleo katika Mkoa wa Pwani kwa kuwekeza si tu katika uzalishaji, bali pia katika ustawi wa jamii kwa kupitia ajira, miradi ya kijamii na ushirikiano wa karibu na wadau wa Sekta ya Madini na maendeleo ya jamii,” ameeleza.

Pesatu ni jukwaa la habari, elimu ya kifedha, na ujasiriamali Tanzania. Tunakuletea taarifa mpya za biashara, uwekezaji, ajira, kilimo, mitindo, na burudani, pamoja na mwongozo wa kufanikisha mafanikio yako. Kwa makala zetu, mwongozo wa vitendo, na taarifa za hivi punde, tunasaidia wajasiriamali, vijana, na jamii kupata maarifa yanayoweza kubadilisha maisha yao na kuongeza fursa za kifedha.

Jarida la Habari

PESATU – Haki Zote Zimehifadhiwa. Imetengenezwa na Mediapix Limited