Home BIASHARAUWEKEZAJI Tanzania yasaini mkataba mpya wa ubia na nchi za OACPS, EU

Tanzania yasaini mkataba mpya wa ubia na nchi za OACPS, EU

0 comments 686 views

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesaini Mkataba Mpya wa Ubia baina yake na Nchi Wanachama wa Caribbean, Afrika na Pacific (OACPS) kwa upande mmoja na Umoja wa Ulaya (EU) na Nchi Wanachama wake, kwa upande mwingine.

Mkataba huo umesainiwa na Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji Jestas Abuok Nyamanga kwa niaba ya Serikali ya Tanzania katika Makao Makuu ya Sekretarieti ya Jumuiya ya Nchi za OACPS.

Mkataba huu unachukua nafasi ya Mkataba wa Ubia wa Cotonou uliosainiwa mwaka 2000, ambao utafikia ukomo wake tarehe 31 Desemba 2023.

Hivyo, kuanzia Januari 1, 2024, Mkataba huu mpya uliopewa jina la Samoa ndiyo utakuwa msingi wa kisera na kisheria kuongoza ushirikiano na ubia na EU kwa kipindi kijacho.

Maeneo muhimu ya ushirikiano katika Mkataba huu ni pamoja na ukuaji wa uchumi na maendeleo endelevu, biashara na uwekezaji, utunzaji wa mazingira na kukabaliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, kukabiliana na matishio mapya ya amani na usalama, uhamiaji, demokrasia na haki za bianadamu.

Itakumbukwa kuwa, ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya Tanzania na EU ulioanza rasmi mwaka 1975, umekuwa ukijengwa katika mikataba ya ubia ambayo imekuwa ikisainiwa baina ya nchi za OACPS na EU.

Ni kupitia mikataba hii ya Ubia, Tanzania imekuwa ikinufaika kwa kiasi kikubwa kwenye ushirikiano wake na EU, katika maeneo mbalimbali, ikiwemo biashara, uwekezaji, utalii, misaada ya maendeleo na maeneo mengine.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje inasema “kwa mfano, katika kipindi cha kuanzia mwaka 1997 mpaka mwaka 2022, Tanzania ilipokea kutoka EU uwekezaji wenye thamani ya Dola za Marekani zaidi ya billion 3.4. Kwa upande wa biashara, mauzo ya bidhaa za Tanzania katika soko la EU yameendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka, ambapo mpaka kufikia mwaka 2021 yalifikia Dola za Marekani milioni 891.5.”

Aidha, tangu kuanzishwa kwa ubia huo, Tanzania imepokea kutoka EU msaada wa zaidi ya Euro bilioni 2.3, sawa na shilingi trilioni 6.3 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.

Pesatu ni jukwaa la habari, elimu ya kifedha, na ujasiriamali Tanzania. Tunakuletea taarifa mpya za biashara, uwekezaji, ajira, kilimo, mitindo, na burudani, pamoja na mwongozo wa kufanikisha mafanikio yako. Kwa makala zetu, mwongozo wa vitendo, na taarifa za hivi punde, tunasaidia wajasiriamali, vijana, na jamii kupata maarifa yanayoweza kubadilisha maisha yao na kuongeza fursa za kifedha.

Jarida la Habari

PESATU – Haki Zote Zimehifadhiwa. Imetengenezwa na Mediapix Limited