Wananchi watakiwa kutoa taarifa za wakopeshaji wasio rasmi

Screen Shot 2025 02 04 at 1.02.47 PM

Wajasiliamali na wananchi wa Wilaya ya Monduli mkoani Arusha, wametakiwa kutoa taarifa kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Kata zao kuhusu wakopeshaji wasio rasmi wanaokopesha kinyume na taratibu na Sheria za Huduma Ndogo za Fedha ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.

Wito huo umetolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli mkoani Arusha, Dkt. George Kasibante, alipotembelewa na kufanya mazungumzo na Timu ya Wataalam wa Kutoa Elimu ya Fedha, kutoka Wizara ya Fedha na Taasisi zake kabla ya Timu hiyo kuelekea katika maeneo mbalimbali ya Wilaya hiyo kutoa elimu ya fedha kwa wananchi.

Alisema utoaji taarifa juu ya uwepo wa watoa huduma za fedha wasiokuwa waaminifu utasaidia Serikali kuwatambua na kuwachukulia hatua za kisheria na kuwafanya watoa huduma hao kufuata Sheria za Huduma Ndogo za Fedha ikiwemo kusajiliwa rasmi na kuleta unafuu wa kukopa kwa wananchi na kukuza kipato chao.

‘’Naamini hawa watu tunaishi nao majumbani, wengine ni wakopeshaji ambao wengine hawatambuliki kwa hiyo wito wangu kwa wananchi kama wakibaini kuna watu wa namna hiyo basi watoe taarifa kwenye Ofisi za Kata zao’’ alisema Dkt. Kasibante.

Aliipongeza Wizara ya Fedha kwa kuendelea kutoa elimu ya fedha kwa umma kwakuwa mafunzo hayo yanawafanya wananchi kupata uelewa juu ya matumizi sahihi ya fedha, masuala ya mikopo na kuwakwamua kiuchumi huku akishauri zoezi hilo kuwa endelevu.

Akitoa elimu ya fedha kwa wananchi wa Monduli, Afisa Usimamizi wa Fedha, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Salim Khalfan Kimaro, amewasisitiza wahamasishaji wa vikundi vya huduma ndogo za fedha kujisajili na kushiriki mafunzo mbalimbali yanayotolewa ili kuwa wabobezi kuhusu masuala ya fedha huku akiwaasa wajasiliamali kuhakiki usajili wa wahamasishaji wa vikundi vyao.

‘’ Waulizeni wale wahamasishaji mnaowaita walimu wa vikundi mwenzetu umesajiliwa tunaomba tuone cheti chako, kwa sababu mkiwa na wahamasishaji ambao hawana elimu ya uhamasishaji wa masuala ya fedha ataelekeza kinyume na taratibu’’ Alisema Bw. Kimaro.


Discover more from PesaTu – Habari za Biashara na Uchumi Tanzania

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Discover more from PesaTu – Habari za Biashara na Uchumi Tanzania

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading

Enable Notifications OK No thanks