Maeneo ya kiuchumi yanavyowainua vijana,Katika kipindi cha sasa ambacho idadi ya vijana inaongezeka kwa kasi,suala la ajira na uwezeshaji wa kiuchumi limeendelea kuwa ajenda muhimu ya kitaifa. Uanzishwaji wa maeneo ya kiuchumi maalumu kwa vijana umeibuka kama mkakati madhubuti wa kukuza ajira, ubunifu na maendeleo jumuishi, huku ukiwawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika uchumi wa nchi.
Maeneo ya kiuchumi kwa vijana hurejelea maeneo maalumu yanayotengwa na kuandaliwa kwa miundombinu rafiki ili kuwapa vijana fursa ya kuanzisha na kuendeleza shughuli za uzalishaji, biashara, teknolojia na huduma.
Maeneo haya yanaweza kujumuisha vituo vya ubunifu (innovation hubs),maeneo ya viwanda vidogo na vya kati, masoko ya kisasa, pamoja na kumbi za mafunzo ya ujasiriamali na ufundi stadi.
Uanzishwaji wa maeneo haya unalenga kupunguza changamoto kuu zinazowakabili vijana, zikiwemo ukosefu wa mitaji, maeneo ya kufanyia kazi,ujuzi wa kibiashara na masoko ya uhakika. Kupitia mpangilio huu, vijana huunganishwa na taasisi za kifedha,wadau wa maendeleo na masoko, hali inayowapa nafasi ya kukuza biashara zao kwa uendelevu.
Kwa upande wa Serikali,uanzishwaji wa maeneo ya kiuchumi kwa vijana ni utekelezaji wa sera na mipango ya maendeleo inayolenga kuwawezesha vijana kiuchumi.
Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali imekuwa ikiwekeza katika miundombinu kama umeme, maji, barabara na TEHAMA, ili kuvutia uwekezaji na kuwezesha shughuli za uzalishaji kufanyika kwa ufanisi.
Mbali na ajira, maeneo haya yanakuza ubunifu na matumizi ya teknolojia miongoni mwa vijana. Kupitia mafunzo na ushirikiano na wataalamu, vijana hupata fursa ya kubuni bidhaa na huduma zenye ushindani katika soko la ndani na kimataifa. Hii huchochea ongezeko la thamani ya bidhaa (value addition) na kupanua wigo wa uchumi wa viwanda unaoongozwa na vijana.
Hata hivyo, mafanikio ya maeneo ya kiuchumi kwa vijana yanahitaji usimamizi bora, sera rafiki na ushiriki wa moja kwa moja wa vijana wenyewe. Ni muhimu kuhakikisha kuwa maeneo haya hayabaki kuwa miradi ya muda mfupi, bali yanakuwa mifumo endelevu inayowezesha vijana kwa muda mrefu.
Kwa ujumla, uanzishwaji wa maeneo ya kiuchumi kwa vijana ni chachu muhimu ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Endapo yataendelezwa kwa mpangilio mzuri, ushirikishwaji na uwazi, maeneo haya yana uwezo mkubwa wa kuibua kizazi cha vijana wabunifu, wenye ajira na mchango chanya katika maendeleo ya taifa.
WAZIRI NANAUKA KATIKA UZINDUZI WA JUKWAA LA VIJANA

Joel Nanauka Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana,anasema Serikali imeanza kutekeleza uanzishwaji wa maeneo ya kiuchumi kwa vijana katika meneo mbalimbali nchini ambayo ni maalumu kwa uwekezaji.
Pia amesema serikali chini ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan,imeendelea kushirikisha vijana katika zabuni na manunuzi ya serikali ambapo jumla ya zabuni zenye thamani ya sh. bilioni 10.8 zilitolewa kwa vijana katika kipindi cha mwaka jana.
Nanauka amesema kwa sasa Serikali imeanza kutekeleza kwa vitendo ajenda ya kuanzisha maeneo maalumu ya kiuchumi kwa vijana.”Mpango huu ni makakati mahususi wakuongeza ushiriki wa vijana kuhusika katika uzalishaji.”Kupitia mpango wa maeneo ya kiuchumi ya uwekezaji kwa vijana, serikali imelenga kuwezesha kuanzisha jumla makampuni 20,000 ambayo yatakuwa katika maeneo ya uwekezaji ambao upo chini ya vijana.
AKIZUNGUMZA KUHUSU MIKOPO YA ASILIMIA 10

Nanauka anasema katika kipindi cha mwaka jana vijana wamenufaika na jumla ya sh.bilioni 36.4 ambazo zilitolewa kama mikopo isiyokuwa na riba.
Anasema Maofisa Maendeleo ya Vijana wa Mikoa wanatakiwa kuhakikisha wanashirikiana na vijana katika maeneo yao katika kutafuta fursa kupitia sekta binafsi.”Jukwaa la vijana alilozindua ni la kimkakati ambalo litatoa fursa kwa vijana kusikika, kutoa maoni yao na kupata nafasi ya kujua fursa zilizopo.
”Serikali itahakikisha maoni yatakayokuwa yanatolewa kupitia jukwaa hilo yanachakatwa, yana nakiliwa na kufanyiwa kazi kwa wakati,”anasema
Nanauka anasema serikali inaendelea kuimarisha ujuzi kwa vijana kupitia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), nakukuza ubunifu wa kidijitali.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana Jenifer Omolo,anasema jukwaa hilo lililozinduliwa linalenga kuhakikisha vijana wanapata nafasi ya kusikilizwa kwa ukaribu
Pia anasema jukwaa hilo litasaidia vijana kuunganishwa na sekta binafsi, wadau mbalimbali wa maendeleo na kuwasaidia kujua fursa za kiuchumi na kijamii.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo anasema, serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam umeendelea kushirikiana kwa karibu na vijana katika kuzifikia fursa mbalimbali.

Discover more from PesaTu – Habari za Biashara na Uchumi Tanzania
Subscribe to get the latest posts sent to your email.

