Benki ya CRDB imezinduzi hati fungani ya Al-Barakah Sukuk inayozingatia misingi ya Shari’ah inayounga mkono jitihada za Serikali katika kupanua wigo wa huduma jumuishi za fedha.
Naibu Gavana wa Uthabiti na Usimamizi wa Sekta ya Fedha Sauda Msemo, kwa niaba ya Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ameipongeza CRDB kwa hatua hiyo wakati wa hafla ya uzinduzi wa hati fungani hiyo Agosti 09, 2025 jijini Dar es Salaam ambapo mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete.

Naibu Gavana wa Uthabiti na Usimamizi wa Sekta ya Fedha wa Benki Kuu ya Tanzania Sauda Msemo
“Napenda kuipongeza Benki ya CRDB kwa mchango wao mkubwa katika maendeleo ya uchumi wa Taifa. Mchango huu unajumuisha uwezeshaji wa sekta binafsi kupata mikopo kwa riba na masharti nafuu, pamoja na ubunifu wa bidhaa na huduma mpya za fedha kama hati fungani ya Al-Barakah Sukuk,” alisema Msemo.
Ameeleza kuwa hadi kufikia tarehe 30 Juni 2025, jumla ya benki tano nchini zinatoa huduma za fedha zinazofuata misingi ya Shari’ah.
“Idadi ya akaunti za amana kwa misingi hiyo imeongezeka kutoka 223,081 mwezi Juni 2020 hadi 809,105, sawa na ongezeko la asilimia 263. Aidha, thamani ya amana imepanda kutoka shilingi bilioni 440 hadi shilingi trilioni 1.4, ongezeko la asilimia 216,” alisema.
Msemo pia amebainisha kuwa Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania imechukua hatua mbalimbali za kuimarisha usalama na ustahimilivu wa sekta ya kibenki, ikiwemo kufanya marekebisho ya Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2006, Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006, na Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018. Marekebisho hayo yalipitishwa na Bunge tarehe 30 Juni 2024.
Aidha, ameeleza kuwa Benki Kuu imekamilisha maandalizi ya Kanuni za Uendeshaji wa Huduma za Kibenki Zisizotoza Riba (Non-Interest Banking Business Regulations), ambazo zinatarajiwa kuanza kutumika katika miezi michache ijayo.
Amesisitiza kuwa dhamira ya Benki Kuu ni kuendelea kusimamia kwa karibu sekta ya fedha na kushirikiana na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) ili kuweka mazingira bora kwa utoaji wa hati fungani za Sukuk, hatua itakayochochea zaidi ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Taarifa ya CRDB inaeleza kuwa hatifungani hiyo inalenga kuwezesha biashara bila kutoza riba ikifuata misingi ya Sharia, ambapo hatua kubwa kwa maendeleo ya sekta ya fedha katika Taifa letu.
“Tunawashukuru wateja, wawekezaji na viongozi serikali, sekta binafsi na dini waliohudhuria na kushiriki nasi katika uzinduzi wa CRDB Al-Barakah Sukuk.”
Hii ni fursa ya kila Mtanzania kujiunga kuwekeza kwenye hatifungani hii ili kupata fedha zitakazosaidia kuwezesha biashara bila kutoza riba hususan katika eneo la biashara ndogo na za kati (SME), ” inaeleza taarifa hiyo.
CRDB imesema huo ni uwekezaji salama unaozingatia misingi ya Sharia na kuleta faida kwa jamii na Taifa letu kwa ujumla huku wawekezaji wakiruhusiwa kuwekeza kuanzia shilingi 500,000 au dola 1,000 za Marekani.
Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Sharia inayosimamia huduma za Benki ya CRDB zinazofata misingi ya Sharia (CRDB Al Barakah Banking), Abdul Van Mohamed amesema bodi yake itaendelea kutoa miongozo inayochochea ubunifu ili kuhakikisha huduma zinazotolewa zinaendelea kuongeza ujumuishi wa Watanzania katika huduma za fedha.

Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Sharia inayosimamia huduma za Benki ya CRDB zinazofata misingi ya Sharia (CRDB Al Barakah Banking), Abdul Van Mohamed.
Soma: CRDB Benki yazindua kampeni ya kusogeza huduma karibu na wateja
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema CRDB Al-Barakah Sukuk ni hatifungani ya kipekee inayolenga kukusanya fedha zitakazowezesha biashara bila kutoza riba, hatua inayopanua wigo wa huduma jumuishi na kuchochea maendeleo ya sekta ya fedha nchini.
Nsekela amewashukuru wawekezaji waliothibitisha kuwekeza katika hatifungani hiyo wakiongozwa na Shirika la Maendeleo ya Fedha la Uingereza (British International Investment) na iTrust. Shukrani za kipekee pia amezielekeza kwa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) na Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) kwa ushirikiano wao wa karibu katika kufanikisha hatua hii.
“Kwa pamoja, tunaendeleza dhamira ya kuongeza ushiriki wa Watanzania katika masoko ya mitaji na dhamana, tukichochea ukuaji wa uchumi na ustawi wa Taifa letu.
Uuzaji wa awali hatifungani hii umeanza jana na utahitimishwa Septemba 12 na kisha kuorodheshwa katika soko la hisa la Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela
Mgeni Rasmi ambae ni Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ameipongeza Benki ya CRDB kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana kwenye mauzo ya “Kijani Bond” na “Samia Miundombinu Bond”.
Amesema mafanikio ya hatifungani hizo yanatoa taswira kuwa hata CRDB Al Barakah Sukuk itapata mafanikio makubwa kwani wawekezaji wana imani katika malengo na uwezo wa Benki ya CRDB.
Aidha, Dkt. Jakaya Kikwete ameeleza kuwa CRDB Al Barakah Sukuk itaongeza mchango katika ushiriki wa Watanzania kwenye masoko ya mitaji na dhamana kwa kuwa inatoa nafasi kwa watu ambao awali walikuwa hawawezi kuwekeza kwenye hatifungani zenye riba kwa sababu ya imani zao kuweza kuwekeza katika hatifungani hii.

Rais mstaafu wa awamu ya nne Jakaya Mrisho Kikwete