Benki ya Dunia yaipongeza Tanzania

Screen Shot 2025 04 28 at 12.05.15 PM

Benki ya Dunia (WB) imeimwagia sifa Tanzania kwa usimamizi mzuri wa uchumi wa nchi na kuwa nchi ya kupigiwa mfano barani Afrika licha ya misukosuko mbalimbali ya kiuchumi inayoikabili dunia.

Pongezi hizo zimetolewa na Makamu mpya wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini, Dkt. Ndiamé Diop, alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Tanzania, unaoongozwa na Waziri wa Fedha Dkt. Mwigilu Nchemba kwenye Mikutano ya Majira ya Kipupwe ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia, Jijini Washington D.C, nchini Marekani.

Screen Shot 2025 04 28 at 11.26.54 AM

Dkt Diop alisema kuwa Tanzania ni nchi ya mfano katika usimamizi wa sera za uchumi na fedha ambapo licha ya changamoto za UVIKO 19 na mizozo ya kisiasa inayoendelea sehemu mbalimbali duniani, tathimini ya Benki hiyo inaonesha kuwa uchumi wa Tanzania uko imara ikilinganishwa na nchi nyingine nyingi za Afrika.

Alisifu pia mikakati iliyowekwa na Serikali kwa ajili ya kukabiliana na changamoto ya Sera za nje za Marekani na duniani kwa ujumla za kupunguza misaada na kuondoa ufadhili katika miradi mbalimbali ikiwemo sekta ya afya, kwa kutumia fedha zake za ndani.

Aidha, alipongeza uhusiano imara uliopo kati ya Tanzania na Benki ya Dunia na kuahidi kuwa Benki yake itaendelea kuisaidia Tanzania katika jitihada zake za kukuza uchumi na kuwaondolea umasikini wananchi wake kwa kusaidia fedha zitakazotumika kutekeleza miradi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii pamoja na kutoa misaada ya kiufundi itakayochochea ukuaji wa uchumi.

Kwa upande wake, Waziri wa Fedha Dkt. Nchemba alimweleza Dkt. Diop, kwamba Benki ya Dunia ni mdau mkubwa wa maendeleo wa Tanzania.

Alisema kuwa, usimamizi mzuri wa uchumi unatokana na mwongozo na maono makubwa ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye ameelekeza fedha nyingi katika sekta za uzalishaji na maendeleo ya jamii lakini pia ujenzi wa miundombinu inayochochea ukuaji wa uchumi.


Discover more from PesaTu – Habari za Biashara na Uchumi Tanzania

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Discover more from PesaTu – Habari za Biashara na Uchumi Tanzania

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading

Enable Notifications OK No thanks