Home VIWANDANISHATI Ukuaji Sekta ya Madini waongeza mahitaji ya umeme Tanzania: Dkt. Biteko

Ukuaji Sekta ya Madini waongeza mahitaji ya umeme Tanzania: Dkt. Biteko

0 comments 56 views

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, amesema ongezeko la shughuli za uchimbaji na uongezaji thamani sekta ya madini limechochea mahitaji makubwa ya nishati ya umeme nchini, hali inayothibitisha kasi ya ukuaji wa sekta hiyo.

Amebainisha hayo Septemba 28, 2025, wakati akihitimisha Maonesho ya 8 ya Teknolojia ya Madini yaliyofanyika mkoani Geita, katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan Bombambili kuanzia Septemba 18 hadi 28 2025.

Ukuaji Sekta ya Madini waongeza mahitaji ya umeme Tanzania: Dkt. Biteko pesatu.co.tz

Dkt. Biteko amesema Serikali inaendelea kupeleka nishati ya umeme kwenye maeneo ya uchimbaji pamoja na viwanda vya kusafisha na kuongeza thamani madini ili kuhakikisha uzalishaji hausimami na kuongeza tija.

“Ukuaji wa Sekta ya Madini unakwenda sambamba na ongezeko la mahitaji ya nishati ya umeme nchini, mfano hapa Geita megawati zaidi ya 30 zinatumika hapa tofauti na hapo awali.

Serikali imejipanga kuhakikisha umeme unaendelea kufika kwenye migodi, maeneo ya wachimbaji wadogo na viwanda vya uongezaji thamani ili sekta iendelee kukua kwa kasi na kutoa ajira zaidi,” ameeleza Dkt. Biteko.

Dkt. Biteko amesema mageuzi ya teknolojia na usimamizi madhubuti katika sekta ya madini, yameiwezesha serikali kukusanya sh3.8 trilioni katika kipindi cha miaka minne, sawa na asilimia 96 ya lengo la Wizara ya Madini.

Dkt. Biteko amesema mabadiliko hayo yamejidhihirisha zaidi kwa wachimbaji wadogo, ambao mchango wao umeongezeka kutoka asilimia 20 mwaka 2020 hadi asilimia 40 mwaka 2024, huku mapato yao yakiongezeka kutoka asilimia 6.8 hadi asilimia 10 katika kipindi hicho.

Amesema katika Mkoa wa Geita pekee, wachimbaji wadogo wamezalisha kilo 22,000 za dhahabu zenye thamani ya Sh trilioni 3.43 na kuiingizia serikali mapato ya zaidi ya Sh2.5 bilioni kati ya mwaka 2021 na 2025.

Kutokana na mafanikio hayo, serikali imeanzisha masoko ya madini 43 na vituo vya ununuzi 109 ili kurahisisha biashara na kuongeza ushiriki wa Watanzania katika mnyororo wa thamani kuanzia utafiti, uchimbaji, uchenjuaji hadi biashara.

Amesema katika kukuza sekta hiyo na kuongeza thamani ya madini yanayozalishwa , viwanda nane vya uchenjuaji na usafishaji madini vimeanzishwa nchini kwa ajili ya dhahabu, shaba na nikeli, hatua inayolenga kuongeza thamani ya madini ndani ya nchi.

Dkt. Biteko ameongeza kuwa Sekta ya Madini imeendelea kuwa himilivu katika kipindi cha miaka minne na kwa sasa imejidhihirisha kama moja ya mihimili muhimu ya kiuchumi nchini.

Soma: Sekta ya madini yafikia mchango wa 10.1% Pato la Taifa

Awali, alipokuwa akitembelea mabanda katika Maonesho hayo, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilieleza kuwa tayari imenunua zaidi ya tani 10 za dhahabu zenye thamani ya shilingi trilioni 2.5, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha akiba ya taifa na kulinda uchumi dhidi ya misukosuko ya kimataifa.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo, alisema tangu kuanzishwa kwake miaka minane iliyopita, Maonesho ya Teknolojia ya Madini Geita yameleta manufaa makubwa kwa Sekta na taifa kwa ujumla.

“Kupitia maonesho haya tumeona maboresho makubwa kwenye usalama wa migodi na shughuli za uchimbaji, ufanisi na ongezeko la tija,” amesema Mbibo.

Nae Mkuu wa mkoa wa Geita Martine Shigela amesema zaidi ya leseni 9000 zimetolewa kwa wachimbaji wadogo, huku baadhi ya washiriki na wadhamini wakielezea ushiriki wao katika maonesho hayo.

Shigela amesema kuna ongezeko la washiriki 300 kwenye Maonesho ya nane ya Teknolojia ya Madini, ambapo kwa mwaka 2024 kulikuwa na washiriki 600 na mwaka huu wa 2025 kuna washiriki zaidi ya 930.

Ukuaji Sekta ya Madini waongeza mahitaji ya umeme Tanzania: Dkt. Biteko pesatu.co.tz

Mkuu wa mkoa wa Geita Martine Shigela

“Tofauti na mwaka jana, mwaka huu tuna wageni wengi kutoka nje ya nchi. Hatukuwahi kuwa na wageni kutoka Malawi lakini mwaka huu tuna wageni kutoka Malawi zaidi ya 20 ambao wamekuja kujifunza uchimbaji wa madini,” amesema Shigela.

Katika kuboresha zaidi maonesho hayo, Shigela amesema mwaka huu waliweka wanyama ambao waligeuka kivutio kwa watu waliofika kuwaona wanyama hao wakiwemo simba, chui, fisi mamba, nyani, kobe na wengineo.

Soma Zaidi: Wawekezaji waitwa Iringa kuwekeza sekta ya madini

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter

Subscribe my Newsletter for new blog posts, tips & new photos. Let's stay updated!