Mwanafunzi SUA atengeneza kifaa cha kuhifadhi mazao ya bustani

Technology Mwanafunzi SUA atengeneza kifaa cha kuhifadhi mazao ya bustani

Changamoto ya kuoza na kuharibika kwa mazao ya bustani kumewasukuma wanafunzi wabunifu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kuja na ubunifu wa kifaa ambacho kina uwezo wa kutunza mazao hayo kwa muda mrefu zaidi.

Mwanafunzi Christina Josephat anayesoma Shahada ya Sayansi ya Usalama wa Chakula na Uthibiti Ubora, SUA amesema wamekuwa wakiguswa na namna ambavyo wafanyabiashara wanapata hasara ya kuoza kwa mazao ya matunda na mbogamboga kiasi cha kulazimika kuuza hata kwa bei pungufu hasa majira ya joto.

“Tuliguswa sana na hali hiyo, ndipo tulipoanza kuulizana sisi wenyewe kwamba tunaweza kufanyaje, ndipo tukaamua kuja na wazo na kifaa hiki rahisi lakini chenye msaada mkubwa kwa wafanyabiashara wadogo maana hakitumii umeme,” alisema Christina.

Christina ambaye anaiwakilisha Kampuni ya Fruit Secure Solution ambayo imezalisha kifaa hicho anasema ujio wake utakuwa msaada kwani kinauwezo wa kutunza matunda bila kuoza kutoka wastani wa siku 3 hadi 9 jambo ambalo litapunguza hasara na kuongeza tija kwa wafanyabiashara.

Mwanafunzi SUA atengeneza kifaa cha kuhifadhi mazao ya bustani
Mmoja wa wanafunzi waliobuni kifaa cha kuhifadhi matunda na mbogamboga akipokea tuzo.

Kampuni ya Fruit Secure Solution ilitangazwa mshindi wa kwanza katika shindano la ubunifu lililoandaliwa na SUA Innovation Hub, jambo lililothibitisha ubora na mchango wa mradi huo katika sekta ya kilimo na lishe nchini Tanzania.

Akizungumza wakati wa tukio hilo, Lucia Madalla kutoka Kitengo cha Uhaulishaji wa Teknolojia na Kituo cha Ubunifu SUA alisema kuwa kitengo kitaendelea kukuza na kulea wanafunzi wenye bunifu ili waweze kukua na kuleta suluhisho kwa changamoto.

“Tunaendelea kuwalea wanafunzi ili waendeleze bunifu zao kwa manufaa yao binafsi hata kwa taifa kwa ujumla,” alisema Madalla.

Fruit Secure Solution inaendelea kupanua wigo wake katika masoko mbalimbali ya ndani nchini Tanzania, ikiwa ni hatua muhimu kuelekea kupunguza upotevu wa chakula na kulinda mazingira.

Pia unaweza kutumia njia nyingine ili kuepusha matunda na mboga kuoza haraka kwa kufuata miongozo hii ya uhifadhi na utunzaji:

Uhifadhi Sahihi

Uhifadhi sahihi ni pamoja na kuweka mazao ya mbogamboga na matunda kwenye jokofu (Friji). Kwa mboga na matunda yanayoanza kuoza haraka kama vile mchicha, zabibu na mengineyo.

Mazao mengine kama vile viazi, vitunguu, vitunguu saumu, ndizi, na nyanya yanaweza kuwekwa kwenye joto la kawaida.

Pia kwa mazao ya mbogamboga unashauriwa unapoyaweka kwenye jokofu uyaweke katika kifungashio kilichofungwa vizuri na matunda yawekwe kwenye sehemu yenye hewa.

Njia nyingine ni kutenganisha mazao

Hapa ni kutenganisha mazoa na yale yanayochangia mazao mengine kuoza.

Kama ulikuwa hufahamu basi leo fahamu. Kuna aina ya matunda yakichanganywa pamoja hupelekea matunda mengine kuiva haraka na kuoza haraka pia. Mfano ndizi na parachichi.

Matunda yanayotoa Ethylene (yanayofanya mengine kuoza haraka).

Miongoni mwa matunda hayo ni ndizi, mapera, parachichi, nyanya, zabibu.

Mbogamboga zinazoathirika zaidi na Ethylene: Mchicha, kabichi, spinachi, carrots, berries. Hivyo unashauriwa kuzitenga na nyingine.

Epuka Unyevu na Ukungu

Ikiwezekana usioshe matunda unapoyahifadhi. Bali uyaoshe pale unapotaka kula. Matunda kama zabibu na jamii inayofanana na zabibu unaweza kuosha kwa kutumia vinegar.

Pia unaweza kutumia vitambaa au karatasi kwa kuweka ndani ya chombo unachohifadhia matunda au mbogamboga ili kuzuia na kunyonya unyevu ambao hupelekea mazao hayo kuharibika haraka zaidi.

Pia katika utunzaji wako wa kuweka katika vifungashio unaweza kutumia vifungashio/mifuko yenye matobo.

Tumia njia nzuri ya kufunga

Kwa matunda/mboga zilizokatwa weka kwenye vyombo vilivyofungwa vizuri kama vile contena zenye mifuniko.

Funga mazao yaliyokatwa nusu kama vile kitunguu kwa mfuko wa kufungia vyakula.

Pia unaaweza kuweka karoti kwenye maji kama huna jokofu ili ziendelee kuwa freshi.

Njia ya kugandisha kwenye jokofu

Kwa wale wenye uwezo wa kumudu kuwa na jokofu linalogandisha (freezer) unaweza kutumia njiaa hii.

Hifadhi Kwenye Baridi ya Sana (Freezer)

Hapa unachemsha mboga kwanza (kama vile maharage, njegere hata baadhi ya mboga za majani na kuziweka katika freezer ili kuzigandisha.

Njia nyingine ya kuzuia kuoza kwa mazao hayo ni kuyaangalia mara kwa mara

Kwa kuyaangalia mara kwa mara itasaidia kubaini mazao yalioanza kuharibika na kuyatoa ili yasifanye mengine kuoza.

Nunua mazao freshi

Hapa zingatia kununua mazao yaliyovunwa hivi karibuni. Mazao yaliyovunwa hivi karibuni yanaweza kuhifadhiwa kwa muda mrefu ukilinganisha nay ale yaliyovunwa mda mrefu.

Pia upuka kununua au kukata matunda ambayo huyatumii kwa muda huo. Kukata matunda pasipo kutumia kwa muda huo na kuyaacha kwa muda mrefu hupelekea matunda kuharibika kwa haraka.

Hizo ni baadhi ya mbinu ambazo zitakusaidia kutunza mazao yako ya mbogamboga na matunda. Pia unaweza kutumia mbinu nyingine kulingana na aina ya mazao pamoja na mazingira ya hali ya hewa kulingana na eneo ulilopo.


Discover more from PesaTu – Habari za Biashara na Uchumi Tanzania

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Discover more from PesaTu – Habari za Biashara na Uchumi Tanzania

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading

Enable Notifications OK No thanks