Mgombea Urais wa Tanzania kupitia tiketi ya Chama cha Union for Multiparty Democracy (UMD), Mwajuma Noty Mirambo ameahidi kukuza uchumi endapo atashinda nafasi ya kuwa Rais.
Akiwa ameambatana na Mgombea mwenza wake aitwaye Mashavu Alawi Haji, Mirambo ametoa ahadi hiyo August 11, 2025 wakati akichukua fomu ya Urais katika Tume Huru ya Uchaguzi Jijini Dodoma.
“Endapo Watanzania watanichagua kuwa Rais sisi tutahakikisha tunainua uchumi na maisha ya watu yanakuwa bora.
Sisi kama UMD tunawaomba Watanzania watupigie kura itapofika wakati wa kupiga kura kwa sababu vipaumbele vyetu ni Rafiki kwa kila Mtanzania mwanamama, kijana, makundi maalum, wafugaji na wakulima,” amesema huku akisisitiza kuwa Watanzania hawatajutia kuzaliwa Tanzania.
Ameeleza kuwa UMD ina sera wezeshi na sera rafiki kwa Mtanzania na zitamgusa kila Mtanzania na kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Mwajuma anakuwa Mgombea wa pili mwanamke wa nafasi ya Urais kuchukua fomu ya kugombea Urais katika Tume Huru ya Uchaguzi baada ya mgombea Urais CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan kuchukua fomu August 09,2025.
Nae mgombea Urais wa Tanzania kupitia Tiketi ya Chama cha African Democratic Alliance Party (ADA- TADEA), Georges Busungu amechukua fomu ya Urais katika Tume Huru ya Uchaguzi Jijini Dodoma August 11,2025 huku akiahidi kuleta mapinduzi ya kifikra, kiuchumi na kiteknolojia kwa Watanzania endapo atashinda na kuwa Rais.

mgombea Urais wa Tanzania kupitia Tiketi ya Chama cha African Democratic Alliance Party (ADA- TADEA), Georges Busungu.
Akiongea na Waandishi wa Habari baada ya kuchukua fomu, Busungu amesema Chama chake kina mtazamo tofauti na mkubwa wa kuleta usawa katika Jamii na kuleta mapinduzi makubwa ya njano, pia mapinduzi ya kiteknolojia wakati huu ambapo Dunia inashuhudia ujio wa Akili Mnemba (AI).
“Chama chetu cha ADA-TADEA ni chama ambacho kina mtazamo kidogo tofauti, mtazamo wake mkubwa ni usawa kwa jamii, na nia kubwa ya kugombea Urais ni kuleta mabadiliko makubwa katika jamii ya wananchi wa Tanzania.
Na kitu cha muhimu, ulimwengu umebadilika, sasa ni ulimwengu wa Akili Mnemba (AI). Kwa hiyo chama cha ADA-TADEA muelekeo wake ni kuleta mapinduzi makubwa ya njano au wazaramo wanaita yellow revolution.
Kwa hiyo mapinduzi ya njano yatashughulika na mapinduzi makubwa ya fikra, mapinduzi ya teknolojia na mapinduzi ya uchumi. Kwa ufafanuzi Zaidi mtapata baadae tukishamaliza kuteuliwa kama wagombea Urais kupitia Tume ya Uchaguzi ya Taifa,” ameeleza Busungu.
Busungu amewasili katika ofisi hizi akiwa ameambatana na wampambe wake na walinzi.
Mgombea mwingine kupitia Chama cha National League for Democracy (NLD), Doyo Hassan Doyo, aliwasili katika ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) akiwa ndani ya usafiri wa Bajaji.
Doyo aliwasili katika INEC akiwa ameambatana na msafara wa wafuasi wake na Wapambe.

Mgombea kupitia Chama cha National League for Democracy (NLD), Doyo Hassan Doyo.

Baada ya kushuka katika Bajaji hiyo, alielekea moja kwa moja katika ofisi za INEC kuchukua fomu za kugombea nafasi ya urais kwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Akizungumza na Waandishi wa Habari muda mfupi baada ya kuchukua fomu, Doyo alisema ameamua kutumia Bajaji ikiwa ni ishara ya kuwaunga mkono vijana wengi wenye Maisha ya kawaida.
“Nimekuja na bajaji kwa sababu ya kuwaunga vijana wengi ambao wanajishughulisha na Maisha ya kawaida katika kusafirisha abiria kwa maana bajaji imekuwa ndo chombo cha usafiri rahisi kwa sasa kwa Watanzania. Kwa hiyo nimeona niwa support ili waone Rais ajae ni jicho lao,” amesema Doyo.
Amesema hiyo ni ishara ya kuenzi usafiri wa umma unaotumiwa na Watanzania wengi, akisisitiza kuwa anataka kuonyesha ukaribu na wananchi atakaowaongoza endapo atashinda uchaguzi huo.
Akijibu swali la mwandishi wa habari alietaka kujua kama ataendelea kutumia bajaji kama akifanikiwa kuingia madarakani, Doyo amesema “mimi nikiingia madarakani gari lolote la serikali lililonunuliwa zaidi ya milioni 200 linauzwa.
Tutafanya mnada, tutatumia magari ya kawaida, yale mashangingi ya milioni mia tatu, mia nne, mia tano nikiwa Rais siwezi kutumia yale, serikali yangu itabana matumizi ili hizo fedha tulizipeleke kwenye miradi kwa sababu miradi mingi inakwama kwa sababu ya fedha. Kwa hiyo nitaendelea kutumia usafiri wa chini kuwafikia Watanzania,” ameahidi Doyo.
Leo August 12, 2025 mgombea wa nafasi ya Rais kupitia Chama Cha Kijamii (CCK), David Mwaijojele amekabidhiwa rasmi fomu za kugombea Urais.

Mgombea wa nafasi ya Rais kupitia Chama Cha Kijamii (CCK), David Mwaijojele.
Baada ya kuchukua fomu, Mwaijojele ametaja moja ya changamoto kubwa kwa watumishi wa umma kuwa ni hofu ya kustaafu, akisema wengi wao hukosa ujasiri wa kuacha kazi hata wanapofikia umri wa kustaafu kwa mujibu wa sheria.
Ameeleza kuwa sababu kuu inayowafanya baadhi ya watumishi wa umma kusita kustaafu ni kutokujua watakwenda wapi au kufanya nini baada ya maisha ya ajira.
“Watu wengi wanaogopa kustaafu kwa sababu hawajajiandaa kisaikolojia wala kiuchumi. Hawajui wataishije au watakaa wapi baada ya kazi. Lakini suluhisho lipo,” amesema Mwaijojele, bila kufafanua kwa undani mapendekezo ya chama chake katika kushughulikia changamoto hiyo.
Mwaijojele ameahidi kuweka wazi mikakati ya CCK kuhusu masuala ya wastaafu katika kampeni zake za urais.
Hata hivyo, Mwaijojele amesema moja ya mikakati ya kuwawezesha watumishi wa umma kunufaika baada ya kustaafu ni kuanzishwa kwa mpango maalumu wa makato ya kodi, ambapo sehemu ya mapato yao itahifadhiwa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za makazi.
