Home BIASHARA Tanzania, Oman zadhamiria kuimarisha ushirikiano wa biashara na uwekezaji

Tanzania, Oman zadhamiria kuimarisha ushirikiano wa biashara na uwekezaji

0 comments 43 views

Tanzania na Oman zimekutana kujadili kuongeza wigo wa ushirikiano katika biashara na uchumi kupitia Jukwaa la Biashara.

Jukwaa hilo lililowakutanisha wafanyabiashara na wadau wa uwekezaji na biashara kutoka Tanzania na Oman limefanyika jijini Dar es Salaam, Oktoba 6, 2025 na kufunguliwa na Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Abdallah Kilima.

Katika hotuba yake, Balozi Kilima amesisitiza kuwa Tanzania na Oman zina nafasi kubwa ya kutumia fursa zilizopo katika sekta za kilimo, mazao ya uvuvi, madini, uwekezaji, utalii, na usafiri wa anga katika kukuza ushirikiano wao wa kibiashara.

Sekta nyingine zinazoenda kunufaika na ushirikiano huo ni pamoja na nishati mbadala na sekta ya Afya.

Naye Balozi wa Oman hapa nchini Tanzania Saud Al Shidhani aliyeongozana na ujumbe kutoka Ofisi ya Taifa ya Mipango wa Sekta binafsi na Ukuzaji Biashara Oman, Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Oman ameeleza kuwa Oman ipo tayari kushirikiana kwa karibu na Tanzania katika sekta mbalimbali ili kukuza biashara na kutengeneza ajira zaidi kwa vijana wa mataifa hayo mawili.

Oman imeainisha maeneo ya kuongeza ushirikiano baina yake na Tanzania ikiwemo kuongeza ushirikiano kati ya sekta binafsi za mataifa yote mawili, sekta ya chakula na usindikaji wa chakula, sekta ya afya pamoja na nishati mbadala ikiwa ni maeneo yanayolandana na vipaumbele vya Tanzania.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Diplomasia ya Uchumi katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi John Ulanga ameeleza kuwa Jukwaa hili ni fursa kwa Tanzania katika kukuza uwekezaji, kuongeza biashara na ajira kwa vijana.

Ameongeza kuwa mauzo ya nje kwa Tanzania yameongezeka mara mbili kwa kipindi cha miaka minne toka dola bilioni 8 hadi dola bilioni 16 ambapo sekta za utalii na uchukuzi ndizo zilizochagiza zaidi ongezeko hilo akiainisha kuwa ipo haja ya kuongeza mauzo zaidi ya bidhaa nje ya nchi.

Wafanyabiashara na wadau mbalimbali kutoka Tanzania wameshiriki katika jukwaa hilo ikiwemo TanTrade, TISEZA, TCCIA na Hill Water.

Katika hatua nyingine, wafanyabiashara wa Oman wamekutana na uongozi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA)

Ujumbe wa wafanyabiashara kutoka Mpango wa Kitaifa wa Maendeleo ya Sekta Binafsi na Biashara za Nje (Nazdaher) wa Oman wametembelea TAA kuangazia fursa za ushirikiano katika usafiri wa anga na ndege za mizigo.

Wafanyabiashara wa Oman wamekutana na uongozi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) pesatu.co.tz

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Kaimu Mkurugenzi wa Biashara na Maendeleo,  Mzee Kilele amesema milango ya TAA iko wazi kuangazia ushirikiano baina ya nchi hizo mbili katika kuwezesha biashara kwa njia ya anga.

Ameongeza kuwa mbali ushirikiano huo ni vyema kuwepo na mpango wa kubadilishana ujuzi wa kitaalamu katika maeneo ya ushirikiano.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato, Clemence Mbaruku ameukaribisha ujumbe huo kuangazia pia fursa mbalimbali za kibiashara na uwekezaji kupitia uwanja huo wenye ukubwa wa kilometa za mraba 45.

Kwa upande wake kiongozi wa msafara, Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa Nazdaher,  Adham Al Ghazali amesema Oman inatazamia ushirikiano huo kukuza sekta za biashara, afya, chakula, nishati mbadala, ushirikiano wa uwili, uwekezaji na kuangazoa zaidi makubaliano ya ushirikiano hapo baadaye kati ya Tanzania na Oman.

Soma: Tanzania, Oman zasaini mkataba kuondoa kodi mara mbili

Watembelea pia Bandari ya Dar es Salaam (TPA)

Watembelea pia Bandari ya Dar es Salaam (TPA) pesatu.co.tz
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Plasduce Mbossa amekutana na ujumbe kutoka Mpango wa Kitaifa wa Maendeleo ya Sekta Binafsi na Biashara za Nje ya Oman (Nazdaher) kuangazia ushirikiano wa kibiashara kati ya Tanzania na Oman kupitia bandari za Tanzania.

Kwa pamoja wamezungumzia fursa za ushirikiano na kwa namna gani kupitia bandari ya Dar es Salaam ambayo ni lango kuu la biashara kwa nchi takriban nane inavyoweza kuongeza na kukuza Biashara kati ya Tanzania na Oman. Aidha, alilisistiza kuwa zipo fursa nyingi ambazo Serikali ya Oman inaweza kuwekeza hususani katika bandari za Mtwara, Tanga, Kigoma na Mwanza .

Aidha, ujumbe huo wa Wafanyabiashara ulipata nafasi ya kuzuru eneo la Bandari ya Dar es Salaam na kujionea namna uendeshaji na usimamizi unavyofanyika chini ya muwekezaji DP World.

Maeneo ya ushirikiano na TPA ni pamoja na usafirishaji wa mazao ya kilimo, usafirishaji wa nyama zilizogandishwa kati ya maeneo mengine mengi.

Watembelea pia Bandari ya Dar es Salaam (TPA) pesatu.co.tz

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter

Subscribe my Newsletter for new blog posts, tips & new photos. Let's stay updated!