Usanifu wa kipekee wa majengo yanayo jengwa katika Hifadhi ya Taifa Ruaha (RNP), yanatarajiwa kuwa kivutio kikubwa kwa watalii wanaotembelea Hifadhi hiyo ya pili kwa ukubwa nchini.
Majengo hayo yanajengwa kupitia Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW).
Hayo yamebainishwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii anaeshughulikia Maliasili, Kamishna wa Polisi Benedict Wakulyamba wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa REGROW, miundombinu pamoja na kutoa mafunzo ya Haki Jinai kwa Maafisa na Askari wa Hifadhi hiyo.
CP. Wakulyamba amesema kuwa Hifadhi ya Taifa Ruaha inakwenda kufunguka zaidi kupitia maboresho makubwa yanayofanyika kupitia Mradi wa REGROW ambao ni matokeo chanya ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwaletea maendeleo watanzania.
Aidha, CP. Wakulyamba ameupongeza uongozi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kwa kusimamia vyema utekelezaji wa mradi huo ndani ya Hifadhi ya Taifa Ruaha hali inayopelekea wakandarasi kufanya kazi kwa kasi ya ujenzi wa majengo na viwanja vya ndege, huku akiuimiza uongozi huo kuendelea kuwasimamia vyema wakandarasi ili miradi ikamilike kwa wakati uliopangwa.
CP. Wakulyamba licha ya kuwapongeza Wakandarasi kwa kazi nzuri wanayofanya ya kufikia hatua inayoridhisha, amewataka kuongeza kasi zaidi ili kukamilisha kazi zao kwa wakati ili watanzania waweze kunufaika na matunda ya mradi huo.
Naye Kamanda wa Kanda ya Kusini – Naibu Kamishna wa Uhifadhi Steria Ndaga kwa niaba ya uongozi wa TANAPA licha ya kuushukuru uongozi wa Wizara chini ya Waziri Balozi Dkt. Pindi Chana kwa ziara hiyo ya Naibu Katibu Mkuu, ameahidi kuhakikisha wanatekeleza maagizo yote yaliyotolewa kwa maslai mapana ya Uhifadhi na Utalii nchini.
Kwa mujibu wa Mhandishi Mshauri wa Majengo Cypriani Mosha, miradi yote 6 imefikia 67% ikihusisha Kituo cha taarifa kwa wageni (VIC) 50%, Hostel kwa ajili ya wanafunzi 72%, majengo ya malazi kwa madereva na waongoza watalii ambayo yamefikia asilimia 73%.
Discover more from PesaTu – Habari za Biashara na Uchumi Tanzania
Subscribe to get the latest posts sent to your email.


