Wachimbaji wadogo wapata fursa mpya. Katika kile kinachoonekana kuwa ni alfajiri mpya kwa wachimbaji wa madini nchini Tanzania, Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini imeweka saini kwenye makubaliano ya kihistoria na Benki ya CRDB.
Yaliyomo
Tukio hili lililofanyika jijini Dar es Salaam , si tu ni hatua ya kiofisi, bali ni ufunguzi wa milango ya kiuchumi ambayo imekuwa ikisubiriwa kwa hamu na maelfu ya Watanzania wanaojishughulisha na uchimbaji mdogo.
Makubaliano haya yanalenga kutatua changamoto ya muda mrefu ya ukosefu wa mitaji, teknolojia duni, na ukosefu wa ushauri wa kitaalamu. Kupitia ushirikiano huu, mfumo wa upatikanaji wa mikopo kwa wachimbaji wadogo sasa umerahisishwa, huku kukiwa na masharti rafiki yanayozingatia uhalisia wa kazi ya uchimbaji badala ya kufuata misingi migumu ya kibenki ya zamani.
Soma zaidi : Wachimbaji wadogo wapata fursa

Maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Utekelezaji wa Wizara
Akizungumza kama mgeni rasmi katika hafla hiyo iliyofanyika kwenye Hoteli ya Johari Rotana, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amebainisha kuwa hatua hii ni utekelezaji wa moja kwa moja wa maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Rais Samia amekuwa akisisitiza kuwa sekta ya madini lazima iwanufaishe Watanzania wenyewe, hususan wale wa hali ya chini na kati.
Waziri Mavunde amemshukuru Rais kwa utashi wake wa kisiasa na uongozi thabiti ambao umeiwezesha Wizara ya Madini kufanya mageuzi makubwa. “Huu ni mwendelezo wa juhudi za makusudi za Serikali kujenga mazingira rafiki kwa wachimbaji wadogo wa madini. Tunataka kuimarisha uchimbaji, biashara, na kuongeza mchango wa sekta hii katika Pato la Taifa (GDP),” alisema Waziri Mavunde.
Serikali imekuwa ikifanya kazi ya ziada kuhakikisha wachimbaji wadogo wanatambuliwa kisheria. Tanzania sasa ni miongoni mwa nchi chache barani Afrika zenye mfumo thabiti wa utoaji leseni kwa wachimbaji wadogo na ufutaji wa leseni za utafiti ambazo hazijaendelezwa ili kutoa nafasi kwa wazawa.
Soma zaidi : Ahadi kwa wachimbaji wadogo

Hatua ya Kihistoria: Mikopo kwa Wachimbaji Wadogo na Rekodi ya Songwe Gold Family
Moja ya habari zilizovuta hisia za wengi katika hafla hiyo ni kutangazwa kwa mkopo wa kishindo kwa kikundi cha wachimbaji. Waziri Mavunde ameeleza kuwa kikundi cha Songwe Gold Family kinakwenda kuandika historia kwa kuwa kikundi cha kwanza cha wachimbaji wadogo kupokea mkopo wa Shilingi Bilioni 50 kwa mkupuo mmoja kutoka Benki ya CRDB.
Hii ni hatua ambayo haijawahi kutokea nchini Tanzania. Kupitia mikopo kwa wachimbaji wadogo ya kiwango hiki, Songwe Gold Family sasa watakuwa na uwezo wa kununua mitambo ya kisasa, kuajiri wataalamu, na kuongeza uzalishaji wa dhahabu kwa kiwango cha viwanda. Hali hii inaondoa dhana kuwa uchimbaji mdogo ni wa kubahatisha na badala yake unageuka kuwa biashara rasmi na yenye tija kubwa.
Pia, Waziri ametoa habari njema kuwa Serikali iko katika hatua za mwisho za kuanzisha Mfuko wa Dhamana (Guarantee Scheme). Mfuko huu utafanya kazi ya kuwa mdhamini kwa wachimbaji wadogo wanapoomba mikopo benki, jambo litakalopunguza kwa kiasi kikubwa vikwazo vya dhamana ambavyo vimekuwa vikiwakwamisha wengi.
Soma kwa undani :Changamoto zinavyotatuliwa za wachimbaji wadogo

CRDB na Mfumo Bunifu wa Dhamana Rafiki
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dkt. Abdulmajid Nsekela, amesisitiza kuwa benki yake imejipanga kikamilifu kuleta mapinduzi. Ameeleza kuwa sekta ya madini imekuwa ikikua kwa kasi kwa miaka mitano mfululizo, hivyo benki haiwezi kubaki nyuma.
“Tofauti kubwa ya mpango huu ni aina ya dhamana. Tumeelewa kuwa mchimbaji mdogo anaweza asiwe na nyumba Masaki au ghorofa Dar es Salaam, lakini ana leseni halali na anachimba dhahabu,” amesema Dkt. Nsekela.
Katika mfumo huu mpya wa mikopo kwa wachimbaji wadogo, CRDB itakubali dhamana zifuatazo:
- Leseni halali za uchimbaji (Mining Licenses).
- Leseni za biashara ya madini (Broker/Dealer Licenses).
- Hifadhi ya madini (Gold Stock) iliyozalishwa.
- Mikataba maalum ya mauzo ya madini.
Hadi sasa, CRDB tayari imeshatoa jumla ya Shilingi Bilioni 186 kwa sekta ya madini, ambapo Bilioni 136 zimeenda kwa wachimbaji wakubwa na Bilioni 50 zimeelekezwa kwa wachimbaji wadogo kupitia mpango huu mpya.
Mchango wa Sekta na Dira ya Taifa 2050
Naye Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya CRDB, Dkt. Donald Mmari, amebainisha kuwa madini ni sekta ya kipaumbele katika Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050. Sekta hii inafungamanisha sekta nyingine kama vile viwanda, usafirishaji, na biashara. Kwa kuwekeza kwa wachimbaji wadogo, Serikali na Sekta Binafsi zinatengeneza mnyororo wa thamani utakaoweza kupunguza umaskini kwa haraka.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo, amempongeza Waziri Mavunde kwa ujasiri wake wa kushawishi taasisi za kifedha. Amesema kuwa kuwashawishi mabenki kuingia “field” na kuona uhalisia wa machimbo kumesaidia kuondoa hofu waliyokuwa nayo hapo awali kuhusu sekta ya madini.
Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Madini Tanzania (FEMATA), John Bina, ametoa neno la shukrani akisema, “Huu ulikuwa kilio chetu cha muda mrefu. Tunamshukuru Rais Samia kwa kutufungulia ukurasa huu mpya. Wachimbaji wadogo sasa hatuendi tena kuomba msaada, tunaenda kuchukua mitaji na kufanya kazi.”
Soma zaidi : Wachimbaji wadogo kuinuliwa kiuchumi

Umuhimu wa Elimu ya Kifedha kwa Wachimbaji
Licha ya kupatikana kwa mikopo kwa wachimbaji wadogo, wadau wamesisitiza kuwa elimu ya kifedha ni muhimu. Benki ya CRDB imeahidi kutoa mafunzo kwa wachimbaji kuhusu jinsi ya kusimamia hesabu zao, kutunza kumbukumbu za uzalishaji, na kuhakikisha mikopo inatumika kwa malengo yaliyokusudiwa. Usimamizi mbovu wa fedha ni adui mkubwa wa maendeleo, na kwa ushirikiano huu, wataalamu wa benki watakuwa bega kwa bega na wachimbaji huko machimboni.
Hii ina maana kwamba mchimbaji wa sasa si yule wa zamani aliyekuwa akipata fedha na kuzitumia bila mpango. Mchimbaji wa sasa ni mfanyabiashara anayefanya kazi na benki, anayelipa kodi, na anayewekeza kwenye teknolojia ili kulinda mazingira na kuongeza tija.
Je, Huu ni Mwanzo wa “Viwanda vya Machimboni”?
Unapozungumzia Shilingi Bilioni 50 kwa kikundi kimoja, hauzungumzii tena habari za jembe na mkoo. Huu ni mwanzo wa kuhamishia viwanda ndani ya machimbo.
TMikopo kwa wachimbaji wadogo inakwenda kuibua tabaka jipya la mabilionea wazawa ambao hawategemei ajira za serikali, bali wanatengeneza ajira maelfu vijijini. Lakini tahadhari ni moja; teknolojia itakayokuja na mikopo hii lazima iambatane na utunzaji wa mazingira. Je, wachimbaji wetu wamejiandaa kugeuka kuwa “Environmental Engineers” huku wakiwa na mifuko iliyojaa mabilioni? Muda utaongea, lakini kwa sasa, mlango wa utajiri uko wazi, na ufunguo wake ni CRDB na Tume ya Madini.
Discover more from PesaTu – Habari za Biashara na Uchumi Tanzania
Subscribe to get the latest posts sent to your email.

