TTFL 2026 Kufungua Fursa za Biashara Tanzania na Dubai.Sekta ya usafirishaji na biashara nchini Tanzania inatarajiwa kupata msukumo mpya kufuatia maandalizi ya Kongamano kabambe la Kimataifa linalolenga kuunganisha masoko ya Afrika Mashariki na Mataifa ya Kiarabu. Taasisi ya Tanzania Freight Forwarders Representation in Dubai (TANFORD) imetangaza rasmi kuandaa kongamano la siku mbili litakalofanyika jijini Dubai, ikiwa ni hatua ya kimkakati ya kuinadi Tanzania kama kitovu cha biashara duniani.
Akizungumza na waandishi wa habari Januari 28, 2026, jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa TANFORD, Hussein Jamal, amebainisha kuwa kongamano hilo linaloitwa Tanzania Trade and Logistics Forum (TTLF) 2026, linatafanyika Februari 13 na 14. Tukio hili linatarajiwa kuwa jukwaa kuu la kutafuta na kutumia fursa za biashara na usafirishaji Tanzania na Dubai.

Kwa Nini Kongamano la TTFL 2026 ni Muhimu kwa Wafanyabiashara?
Lengo kuu la TANFORD ni kuifanya Tanzania kuwa “Gateway” au lango kuu la biashara kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati. Kupitia kongamano hili, wadau wa logistics watapata nafasi ya kuona jinsi miundombinu ya Tanzania—ikiwemo bandari na barabara—inavyoweza kutumika kukusanya mizigo kutoka masoko ya kimataifa na kuisambaza ndani ya bara la Afrika.
“Tumeandaa kongamano hili ili kuinadi nchi yetu kimataifa na kusaidia kukuza matumizi ya bandari zetu. Tunataka kukusanya mizigo kwenye masoko ya kimataifa na kuipitisha Tanzania,”amesema Jamal.
Hii ina maana kuwa, kwa mfanyabiashara mdogo na mkubwa, kuna uwezekano wa kupata mteja wa moja kwa moja kutoka Dubai pasipo kupitia madalali wasio na tija. Kongamano hili ni daraja linalounganisha mahitaji ya bidhaa za Kitanzania na uwezo wa usafirishaji wa kimataifa.

Wadau Muhimu na Ushirikiano wa Serikali
Kongamano hili si la sekta binafsi pekee; ni juhudi za pamoja zinazoungwa mkono na serikali pamoja na mashirika makubwa ya kimataifa. Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Dkt. Latifa Mohammed Khamis, amesisitiza umuhimu wa wafanyabiashara wa ndani kuchangamkia fursa hizi ili kukuza mahusiano ya kibiashara na mataifa ya nje.
Kulingana na Dkt. Latifa, kushiriki katika majukwaa ya kimataifa kama haya hufungua milango ya mashirikiano (partnerships) ambayo mara nyingi hayapatikani ndani ya mipaka ya nchi. Hii ni sehemu ya mkakati wa kukuza fursa za biashara na usafirishaji Tanzania na Dubai kwa vitendo.
Taasisi nyingine nzito zinazotarajiwa kushiriki ni pamoja na:
- TPA (Mamlaka ya Bandari Tanzania)
- TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania)
- DP WORLD
- TAFFA (Chama cha Mawakala wa Forodha)
- TPSF (Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania)
- Makampuni ya usafirishaji kama Silent Ocean na Kilimanjaro Star Cargo.

Logistics: Uti wa Mgongo wa Uchumi wa Tanzania
Rais wa Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TAFFA), Edwin Urio, ametoa takwimu za kutia moyo akisema kuwa sekta ya usafirishaji na logistics iliongoza kwa kuingiza fedha za kigeni nchini katika mwaka wa fedha 2024/2025. Hii inathibitisha kuwa usafirishaji ndio “uti wa mgongo” wa uchumi unaokua.
Kushiriki kwa mawakala wa forodha na wasafirishaji katika kongamano la Dubai kutaongeza ufanisi wa huduma zao, kupunguza gharama za uingizaji mizigo, na kuongeza kasi ya utoaji mizigo bandarini. Hili ni jambo la msingi katika kuimarisha fursa za biashara na usafirishaji Tanzania na Dubai.
Mbinu za Kufaidika na Soko la Dubai
Ili kufanikiwa katika soko la Dubai, wafanyabiashara wa Tanzania wanatakiwa kuzingatia mambo yafuatayo:
- Ubora wa Bidhaa: Masoko ya Dubai yanahitaji viwango vya juu vya ubora, hasa katika bidhaa za kilimo na madini.
- Ufungashaji (Packaging): Bidhaa lazima ziwe na mwonekano wa kuvutia unaoweza kushindana kimataifa.
- Mtandao (Networking): Kongamano la TTFL 2026 ndiyo sehemu sahihi ya kuanzisha mahusiano haya.

Je, Dubai ndiyo Inakuja Tanzania au Tanzania Inaenda Dubai?
Watu wengi wanadhani kongamano hili ni la Watanzania kwenda kutafuta bidhaa Dubai pekee, lakini ukweli ni kinyume chake. Dubai inaitamani Tanzania kwa udi na uvumba. Kwa nini? Kwa sababu Tanzania ina rasilimali ambazo Dubai haina—ardhi yenye rutuba, madini ghafi, na zaidi ya yote, nafasi ya kijiografia (Geopolitical position) inayozipa nchi sita zisizo na bandari uwezo wa kufanya biashara na ulimwengu.
Hivyo, TTFL 2026 si safari ya kitalii; ni safari ya kwenda kuweka sahihi mikataba itakayofanya bandari zetu zifanye kazi saa 24 kwa mizigo itakayolisha nusu ya bara la Afrika. Huu ndio wakati wa kuacha kuwa mnunuzi na kuanza kuwa mtoa huduma wa kimataifa.
Discover more from PesaTu – Habari za Biashara na Uchumi Tanzania
Subscribe to get the latest posts sent to your email.

