Pesatu ni jukwaa la habari, elimu ya kifedha, na ujasiriamali Tanzania. Pata taarifa mpya za biashara, uwekezaji, ajira, kilimo, mitindo, na burudani kwa Kiswahili, pamoja na mwongozo wa kufanikisha mafanikio yako.
PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.
PesaTu inamlenga kila mtu ambaye kwa namna moja au nyingine anaguswa na anapenda kujua/ kufuatilia masuala mbalimbali ya kiuchumi ya nchi ikiwemo ujasiriamali, uwekezaji, viwanda, kilimo na hisa.
Serikali yataka bei bora ya Mahindi mbele ya NFRA.Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Deogratius Ndejembi, ameanza rasmi ziara yake ya kikazi mkoani Ruvuma kwa kutembelea Wilaya ya Mbinga Vijijini.
Yaliyomo
Ziara hii ya Makamu wa Rais Ruvuma imelenga kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, kusikiliza kero za wananchi, pamoja na kutoa maelekezo ya kiutendaji ili kuboresha sekta muhimu za uchumi na huduma za kijamii ikiwemo kilimo, afya, miundombinu ya barabara, na maji.
Akiwa njiani na kuzungumza na wananchi katika maeneo ya Kigonsera na Amani Makoro, Makamu wa Rais amegusa maeneo tete yanayohusu maisha ya kila siku ya wananchi wa mkoa huo unaotambulika kama kapu la chakula la taifa.
Maagizo ya Makamu wa Rais Ruvuma Kwenye Bei ya Mahindi na NFRA
Katika mkutano wa hadhara uliofanyika eneo la Kigonsera, Makamu wa Rais Ruvuma, Deogratius Ndejembi,ametoa agizo zito kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kuhakikisha kuwa mfumo wa upangaji wa bei ya mahindi unazingatia gharama halisi alizotumia mkulima wakati wa uzalishaji.
Agizo hili lilikuja mara baada ya Hoja iliyowasilishwa na Mbunge wa Jimbo la Mbinga Vijijini, ambaye pia ni Waziri wa Viwanda na Biashara,Judith Kapinga. Mbunge huyo alieleza kwa kina changamoto wanazopitia wakulima wa Kigonsera na Mbinga kwa ujumla kutokana na kuyumba kwa bei ya mahindi sokoni, jambo linalowarudisha nyuma kiuchumi licha ya kutumia nguvu na rasilimali nyingi shambani.
Ndejembi alimwelekeza Afisa Mtendaji Mkuu wa NFRA kuweka mikakati thabiti ili katika msimu ujao wa ununuzi, bei itakayowekwa iwe ya kuridhisha na yenye kuwalinda wakulima dhidi ya hasara.
“Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa uzalishaji wa kiasi kikubwa cha mahindi nchini. Tukiwalinda wakulima wa eneo hili kwa kuwapa bei nzuri, hatutakuwa tu tunalinda maslahi yao binafsi, bali pia tutakuwa tunalinda usalama wa chakula wa taifa zima na kuweka uwiano mzuri wa bei katika masoko yetu,” amesisitiza Ndejembi.
Mpango wa Shilingi Bilioni 7.83 Kujenga Eneo la Hifadhi na Kiwanda
Akijibu kero hizo mbele ya Makamu wa Rais, Mbunge wa Mbinga Vijijini, Judith Kapinga, alibainisha kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga imeshachukua hatua za kimkakati ili kutatua adha ya masoko kwa wakulima wa eneo hilo.
Halmashauri inatarajia kutenga eneo maalumu la kuhifadhi mahindi litakaloenda sambamba na ujenzi wa kiwanda cha kuchakata mazao hayo.
Mradi huo mkubwa unatarajiwa kugharimu kiasi cha shilingi bilioni 7.83, hatua itakayosaidia kuongeza thamani ya mahindi na kumpunguzia mkulima adha ya kukosa wanunuzi wakati wa msimu wa kuvuna.
Ukaguzi wa Miradi ya Afya na Miundombinu ya Nyumba za Watumishi
Kabla ya kuzungumza na wananchi kwenye mikutano ya hadhara, Makamu wa Rais alitembelea mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga ili kupokea taarifa ya utekelezaji na kujionea maendeleo ya miundombinu hiyo ya afya.
Katika taarifa iliyowasilishwa, ilielezwa kuwa mwongozo wa Serikali unataka hospitali hiyo kuwa na jumla ya majengo 29. Mpaka sasa, majengo 15 yamekamilika kikamilifu huku majengo 14 yaliyobaki yakiwa katika hatua mbalimbali za ujenzi au mchakato wa fedha.
Elimu ya Utegemezi wa Mapato ya Ndani
Akizungumzia mwenendo wa mradi huo wa hospitali, Mhe. Ndejembi amesisitiza umuhimu wa halmashauri zote nchini kujifunza kutumia mapato ya ndani kutekeleza miradi inayowagusa wananchi moja kwa moja, badala ya kutegemea Serikali Kuu kutoa fedha kwa kila hatua ya maendeleo.
Ili kuhakikisha huduma za afya zinapatikana kwa ufanisi masaa 24, Makamu wa Rais aliagiza Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kutenga angalau shilingi milioni 200 kila mwaka kutoka kwenye mapato yake ya ndani kwa ajili ya kujenga nyumba za watumishi wa afya karibu na hospitali hiyo.
“Watumishi wa afya wakikaa mbali na kituo cha kazi, inakuwa vigumu kutoa huduma za dharura, hususan nyakati za usiku. Kujenga nyumba karibu na hospitali ni uwekezaji wa moja kwa moja kwenye afya za wananchi wenu,” alisema Makamu wa Rais.
Katika kuonyesha kuunga mkono maagizo hayo,Judith Kapinga alieleza kuwa Halmashauri tayari imeelekeza kutengwa kwa shilingi milioni 300 katika mwaka huu wa fedha. Fedha hizo zitazalisha nyumba mbili za watumishi zenye uwezo wa kuhudumia familia tatu kila moja (3 in 1), huku juhudi zingine zikiendelea kutafuta vyanzo vya ziada vya fedha.
Sekta ya Kilimo, Hifadhi ya Mazingira na Barabara za Kimkakati
Katika mikutano yake na wananchi wa Kigonsera na Amani Makoro, Mbunge Kapinga alieleza kwa kina jukumu la sekta ya kilimo katika uchumi wa Wilaya ya Mbinga, akitaja mahindi na kahawa kuwa ndio nguzo kuu za kipato cha wananchi.
Wakulima wa Mbinga wanatumia nguvu na mjirosho mkubwa kuzalisha mazao haya ya chakula na biashara. Kwa sababu hiyo, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kumwaga rasilimali fedha katika maeneo mbalimbali ya Mbinga kuboresha huduma za kijamii kama:
Ujenzi na upanuzi wa hospitali na zahanati
Upatikanaji wa umeme wa uhakika vijijini (REA)
Uboreshaji wa barabara za vijijini na mijini
Ujenzi wa miundombinu ya shule na huduma za maji safi
Kapinga alitumia fursa hiyo pia kuwasihi wananchi kuendelea kuhifadhi mazingira kwa kutunza miti na misitu ya asili ili kulinda vyanzo vya maji vinavyotegemewa sana kwa ajili ya umwagiliaji na matumizi ya nyumbani.
Agizo la Barabara ya Amani Makoro–Ruanda na Sekta ya Maji
Miundombinu ya usafirishaji ilichukua nafasi kubwa katika ziara ya Makamu wa Rais Ruvuma.Ndejembi ameiagiza Wizara ya Ujenzi kuandaa haraka mpango kazi utakaoharakisha ukamilishaji wa ujenzi wa barabara ya Amani Makoro – Ruanda.
Makamu wa Rais ameeleza wazi kuwa barabara hiyo ni kiungo muhimu sana cha kiuchumi. Haibebi tu abiria na mazao ya chakula, bali pia ni njia kuu ya usafirishaji wa makaa ya mawe kutoka migodini.
“Kama mkandarasi aliyepewa kazi ya ujenzi wa barabara ya Amani Makoro–Ruanda ameshindwa kukamilisha mradi kulingana na mkataba, afukuzwe na atafutwe mkandarasi mwingine mwenye uwezo wa kukamilisha kazi hiyo kwa wakati,” aligomea Mhe. Ndejembi.
Pia, ameshauri kuwepo kwa kituo kimoja cha utoaji huduma (One-Stop Center) katika eneo la mizani kwenye barabara hiyo ili kurahisisha utoaji wa huduma za kifedha na kodi, jambo litakaloongeza mapato ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga
Utekelezaji wa Mradi wa Maji Amani Makoro
Kwa upande wa huduma za maji,Judith Kapinga ameishukuru Serikali kuu kwa kutenga kiasi cha shilingi bilioni 1.6 kwa ajili ya mradi wa maji katika eneo la Amani Makoro.
Tayari mkandarasi ameshapokea malipo ya awali ya shilingi milioni 300 ili kuanza kazi mara moja. Fedha zilizobaki zinatarajiwa kutolewa kwa awamu kulingana na maendeleo ya kazi ili kuhakikisha wananchi wa Amani Makoro wanapata maji safi na salama karibu na makazi yao.
Ziara hii ya Makamu wa Rais katika Mkoa wa Ruvuma, iliyomfikisha pia katika Soko Kuu la Songea Mjini, inaonyesha dhamira ya Serikali ya kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kutatua changamoto za wananchi kuanzia ngazi ya chini kabisa.
Je, Bei ya Mahindi Pekee Itamtatulia Mkulima wa Mbinga Umaskini?
Wakati maagizo ya Makamu wa Rais mkoani Ruvuma kwa NFRA yakipokewa kwa furaha kubwa na wakulima wa mahindi wa Kigonsera na Mbinga, kuna ukweli mchungu ambao unastahili kuangaziwa kwa kina: Kupandisha bei ya mahindi pekee sio mwarobaini wa kudumu wa umaskini wa mkulima wa Ruvuma.
Ruvuma imekuwa ikisifiwa kwa miaka nenda rudi kama “kapu la chakula la taifa,” lakini dhana hii imemfunga mkulima katika mtego wa kuzalisha mazao yenye thamani ndogo ya sokoni (low-value commodities).
Mahindi ni zao la chakula kinachotumiwa kwa wingi, lakini faida yake kwa ekari moja ni ndogo ukilinganisha na gharama za pembejeo kama mbolea na mbegu zilizopanda bei duniani.
Kipimo halisi cha kumkomboa mkulima wa Mbinga hakitokani tu na NFRA kununua gunia la mahindi kwa bei ya juu kwa msimu mmoja wa kisiasa. Mtazamo mpya unahitajika katika mambo matatu:
Uboreshaji wa Thamani (Agro-processing): Ahadi ya ujenzi wa kiwanda cha bilioni 7.83 Mbinga ndiyo mbegu halisi ya mabadiliko. Badala ya kusafirisha mahindi ghafi kwenda mikoa mingine au nchi jirani, Mbinga inapaswa kusindika unga, chakula cha mifugo, na wanga (starch).
Kutenganisha Miundombinu ya Makaa ya Mawe na Kilimo: Barabara ya Amani Makoro–Ruanda inapotumiwa na malori mazito ya makaa ya mawe, inaharibika kwa kasi kubwa kuliko uwezo wa halmashauri kuikarabati. Sekta ya madini inapaswa kulipia kikamilifu miundombinu hiyo kupitia kodi za huduma (service levyes) ili fedha za kilimo zisipotee kwenye matengenezo ya barabara.
Utofautishaji wa Mazao (Crop Diversification): Wakulima wa Mbinga wanapaswa kuhimizwa kuongeza uzalishaji wa kahawa na mazao mengine ya biashara yenye soko la kimataifa, badala ya kutegemea mahindi pekee kama zao la kibiashara.