Serikali ya Tanzania kurejesha minada madini ya vito

WhatsApp Image 2024 10 17 at 13.14.28

Serikali kupitia Wizara ya Madini inarudisha minada ya ndani ya madini ya vito itakayofanyika katika maeneo ya uzalishaji.

Maeneo hayo ni pamoja na Mirerani, Mahenge, Tunduru, Dar es salaam, Arusha na Tanga na kimataifa itafanyika mji wa Bangkok na Jaipur nchini Thailand.

Hayo yamesemwa Oktoba 16, 2024 na Waziri wa Madini Anthony Mavunde wakati akijibu hoja mbalimbali zilizoibuliwa na wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Nishati na Madini jijini Dodoma.

Waziri Mavunde amesema kuwa baada ya taratibu za marekebisho ya kisheria kukamilika juu ya uendeshaji wa minada hiyo wanatarajia ndani ya muda mfupi ujao kuanza taratibu za kuweka miundombinu ya kuanza minada ya ndani.

Waziri Mavunde amefafanua kuwa, uendeshaji wa maonesho na minada ya kimataifa nchini ni fursa muhimu ya kutangaza madini ya vito yanayozalishwa hususan kwenye masoko ya kimataifa ambayo ni njia mojawapo ya kuwafikisha watanzania katika masoko ya uhakika na upatikanaji wa bei nzuri na stahiki.

Waziri Mavunde ameieleza Kamati ya Nishati na Madini kuwa, Mpango wa kurejesha minada ya madini ya vito ni utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa ufunguzi wa kiwanda cha kusafisha dhahabu cha jijini Mwanza Juni 13, 2024.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa madini Dkt. Steven Kiruswa amesema kwa sasa wataalam wa Wizara ya Madini wamepata uzoefu mkubwa katika minada na maonesho ya kimataifa baada ya kujifunza namna biashara za kimataifa zinavyofanyika pamoja na matumizi ya teknolojia ya kisasa kwenye mnyororo mzima wa thamani katika nchi mbalimbali ikiwemo Marekani, India, Afrika Kusini na Thailand.


Discover more from PesaTu – Habari za Biashara na Uchumi Tanzania

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Discover more from PesaTu – Habari za Biashara na Uchumi Tanzania

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading

Enable Notifications OK No thanks