Tani 6.5 za dhahabu kutoka kwa wachimbaji wadogo na wakubwa nchini Tanzania zimenunuliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kipindi cha miezi tisa.
Gavana wa BoT Emmanuel Tutuba amesema hayo katika mkutano ambao aliuhudhuria kwa njia ya mtandao na Gavana wa Benki Kuu ya Rwanda (NBR) Soraya Hakuziyaremye, Julai 24, 2025 alipotembelea ofisi za BoT jijini Dr es Salaam.
Gavana Tutuba alimweleza Gavana Hakuziyaremye kuwa “kuhusu ununuzi wa dhahabu BOT ilianza rasmi ununuzi wa dhahabu nchini kuanzia Oktoba 2024 na kufikia Juni 30, 2025 tayari imekwisha nunua tani 6.5 kutoka kwa wachimbaji wakubwa na wadogo.”
Gavana Tutuba amesema Tanzania ina mifumo imara ya malipo ikiwemo TIPS kwa miamala midogo na TISS kwa mikubwa, ambayo ni mifano ya kuigwa na nchi nyingine barani Afrika.
Ameongeza kuwa Benki Kuu inawezesha malipo ya hundi au malipo madogo ya kielektroniki kupitia mfumo wa malipo wa Tanzania Automated Clearing House (TACH), malipo ya nje ya nchi kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kupitia mfumo wa malipo wa East Africa Payment System (EAPS) na inasimamia mfumo wa malipokwa nchi wanachama wa Jumuiya ya maendeleo Kusini mwa Afrika ujulikanao kama SADC RTGS.
Gavana Tutuba amesema BOT na NBR zitaendelea kushirikiana na kujengeana uwezo kwenye maeneo mbalimbali ya sekta ya fedha na uchumi kiujumla ili kuhakikisha nchi zote mbili zinazidi kuimarika katika maeneo hayo.
Kwa upande wake Hakuziyaremye, ameipongeza BOT kwa kutengeneza TIPS kwa kutumia utaalamu wa ndani ya taasisi kitu ambacho kinaonesha ni kwa kiasi gani Benki Kuu imepiga hatua katika eneo hilo.

Gavana wa Benki Kuu ya Rwanda (NBR) Soraya Hakuziyaremye.
Aidha, ameeleza kuwa ushirikiano huu utasaidia kuimarisha udhibiti na usimamizi thabiti wa mifumo ya malipo kwa nchi hizi mbili hususan kutokana na ongezeko la matumizi ya mifumo ya malipo ya kidijitali.
Kikao hiko pia, kilihudhuriwa na Naibu Gavana, Sauda Msemo, Mkurugenzi wa Mifumo ya Malipo ya Taifa, Lucy Shaidi pamoja na wataalamu mbalimbali kutoka BOT.
Msingi wa mazungumzo hayo ulikuwa ni kujadili namna gani Benki Kuu hizi mbili zitashirikiana na kubadilishana uzoefu katika maeneo ya Kusimamia na Kudhibiti Mifumo ya Malipo pamoja na Kuhifadhi Akiba ya Nchi kupitia ununuzi wa dhahabu.
Katika kikao kingine, Gavana Tutuba ameikaribisha Absa Group kupitia kampuni zake kuendelea kuwekeza katika sekta ya fedha nchini.
Gavana Tutuba ameikaribisha Absa Group alipokutana na kufanya mazungumzo na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Absa Group, Kenny Fihla katika ofisi ndogo za Makao Makuu ya Benki Kuu jijini Dar es Salaam Julai 22, 2025.
Akimkaribisha kuwekeza katika sekta ya fedha, Gavana Tutuba amesema, “Tanzania kuna mazingira rafiki ya kufanyia biashara na kuendelea kuimarika kwa uchumi wa Tanzania.”
“Ripoti kutoka Kampuni ya Kimataifa inayojihusisha na kufanya Tathmini ya nchi kukopesheka katika masoko ya mitaji ya kimataifa ya Fitch Ratings inaonesha Tanzania ipo katika daraja la B+ ikiononesha mwenendo mzuri wa uchumi,”ameeleza Gavana Tutuba
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Absa Group, Fihla ambaye ameteuliwa hivi karibuni ameipongeza Benki Kuu kwa usimamizi thabiti wa sekta ya fedha na uchumi wa nchi kiujumla.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Absa Group, Fihla
Absa Group kwa Tanzania pia inamiliki hisa nyingi katika Benki ya NBC.
Mkutano huo pia umehudhuriwa na Naibu Gavana (Uthabiti na Usimamizi wa Sekta ya Fedha), Sauda Msemo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi na Mkurugenzi Mtendaji wa Absa Group kwa ukanda wa Afrika, Saviour Chibiya.