Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania inaendelea kupiga hatua muhimu katika safari yake ya kujenga uchumi wa kisasa unaotegemea maarifa, teknolojia na rasilimali za ndani.
Rais Dkt. Samia maeyasema hayo Julai 30, 2025 wakati akizindua kiwanda cha majaribio cha uchenjuaji wa madini ya Urani kilichopo Wilaya ya Namtumbo mkoni Ruvuma, kinachomilikiwa na kampuni ya Mantra Tanzania Limited.

Rais Dkt. Samia
“Tunataka Watanzania waone manufaa ya moja kwa moja kutoka mradi huu. Ni wajibu wetu kuhakikisha ajira zinazotolewa kwa wananchi hususanwa maeneo yanayozunguka mradi na kwamba mapato yake yanaimarisha huduma za kijamii,” amesema Rais Dkt. Samia.
Aidha, amesema serikali inatambua uwekezaji huo kuwa wa kimkakati unaoweza kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi kwa taifa na wananchi na kuongeza kuwa urani ni rasilimali yenye uwezo wa kuimarisha uchumi, kuzalisha ajira na kuongeza mapato nchini.
Amesma “kiwanda hiki cha majaribio ni sehemu ya utekelezaji wa mikakati yetu ya kuhakikisha tunatumia madini haya kwa manufaa ya Watanzania wote kwa kuzingatia usalama wa kiafya, kimazingira na kufuata viwango vya kimataifa.”

Muonekano wa Kiwanda cha Majaribio cha Kuchenjua Urani cha Mantra Tanzania Limited kilichopo katika Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, kilichozinduliwa na Rais Dkt. Samia
Aliongeza kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi chache barani Afrika zenye akiba kubwa ya madini ya urani ikiwemo hifadhi ya tani 60,000 ya madini hayo katika eneo la Mto Mkuju pekee, jambo linaloliweka Taifa katika rekodi nzuri ya umiliki wa rasilimali hii.
Halikadhalika, Rais Dkt. Samia amesema utekelezaji wa mradio huo ni sehemu ya mkakati wa Dira ya Taifa ya Maeneleo 2050 wa kuifanya Tanzania kuwa taifa lenye viwanda na uchumi wa kati wa juu unaojitegemea na hivyo kuiweka miongoni mwa nchi wachangiaji wakubwa 10 duiniani wa malighafi muhimu na nishati safi ya nyulkia.
Akifafanua manufaa ya kiuchumi, Rais Dkt. Samia amesema uwekezaji wa mradi huo unaokadiriwa kufikia Dola za Marekani Bilioni 1.2, utazalisha Zaidi ya ajira 8,700 za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, huku serikali ikinufaika na mapato takribani Dola bilioni 1 kupitia kodi, mirabaha na gawio kutokana na umiliki wake wa asilimia 20.

Muonekano wa Kiwanda cha Majaribio cha Kuchenjua Urani cha Mantra Tanzania Limited kilichopo katika Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, kilichozinduliwa na Rais Dkt. Samia
Katika hatua nyingine, Dkt. Samia ameitaka kampuni ya Mantra Tanzania Limited kutekeleza mradi huo kwa kuzingatia wajibu wa kijamii wa ushirikishwaji wa Watanzania, huku akizitaka Wizara na Taasisi zinazohusika na usimamizi wa mazingira kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya uenedelevu na usalama wa mazingira.
Vilevile, Rais Dkt. Samia amebainisha kuwa serikali itaendelea kujifunza kupitia uzoefu wa nchi Rafiki kama Jamhuri ya Namibia, ambayo imekuwa ikichimba urani kwa muda mrefu ili kuhakikisha euendelevu wa mradi huo unakwenda sambamba na ulinzi wa mazingira.
Akitolea mfano mataifa yanayozalisha umeme wa urani, Rais Dkt. Samia amesema asilimia 20 ya umeme unaozalishwa nchini Marekani unatokana na madini ya urani huku Ufaransa ikizalisha asilimia 65 ya umeme kutokana na madini hayo.
Nchi nyingine ni Korea Kusini ambayo umeme wake unaozalishwa na urani ni aslimia 30.
Kwa upande wa Bara la Afrika, Rais Dkt. Samia amesema tangu mwaka 1984 Afrika ya Kusini imekuwa mzalishaji pekee wa umeme wa urani.
Ameeleza kuwa, nchi ya Misri inajenga mitambo ya nyuklia kuanza uzalishaji wa umeme wa urani.
Ameishukuru serikali ya Russia kwa fursa hiyo huku akisisitiza fursa za ajira kipaumbele kikubwa wapewe vijana wa maeneo jirani na mradi huo.

Muonekano wa Kiwanda cha Majaribio cha Kuchenjua Urani cha Mantra Tanzania Limited kilichopo katika Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, kilichozinduliwa na Rais Dkt. Samia
Akitoa taarifa za kiwanda hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa Mantra Tanzania Limited Aleksandrs Starikovs amesema kiwanda hicho kitazalisha Zaidi ya ajira 4500 za muda na ajira 700 za kudumu kwa Watanzania.
Amesema “kiwanda hiki katika shughuli mbalimbali kitawezesha takribani ajira 4500 za muda na ajira 700 za kudumu.”
Nae Waziri wa Madini Anthony Mavunde ameitaka Halmashauri ya Namtumbo kuhakikisha wanabuni miradi yenye tija kwa wananchi itakayotekelezwa na kampuni hiyo kupitia utekelezaji wa miradi ya uwajibikaji wa kampuni kwa jamii (CSR).