Mikopo kwa ajili ya boti kubwa za uvuvi ipo mbioni kuanza kutolewa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa wavuvi wa Unguja na Pemba.
Akizungumza akiwa Unguja, Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo Khamis Mbeto Khamis alisema boti hizo ni mbali ya zingine 1500 za kisasa zenye vifaa vyote muhimu, zilizotolewa kwa wavuvi na wakulima wa mwani.
Mbeto alisema boti hizo kubwa za uvuvi za kisasa zitawawezesha wavuvi kufika kina kikubwa cha bahari hivyo kupata samaki wa wengi na kwa uhakika.
Alisema boti hizo wamekabidhiwa zikiwa na jaketi za usalama, rada na kifaa maalum cha kubaini samaki walipo.
“Hivi sasa husikii habari za kupotea wavuvi baharini maana wana rada inayowaongoza sio kama wakati ule wakitumia ngalawa” alisema Mbeto.
Pia wakulima wa mwani hivi sasa wanaenda maji kina badala ya ufukweni hivyo kupata mwani ulio bora sio uliochanganyika na takataka au mchanga.
Sanjari na hilo, ujenzi wa masoko ya samaki yenye vyumba vya baridi (Cold room) kwa ajili ya kuhifadhia umefanyika na iwapo Dkt. Mwinyi atachaguliwa tena, atajenga masoko zaidi ya namna hiyo.
Mbeto alitoa mfano wa soko la samaki Tumbe ambalo lina chumba cha baridi chenye uwezo wa kuhifadhi hadi tani 5,000 za samaki.
“Leo wakausha dagaa wa Ndagoni, Tama na Fungurefu hawaaniki dagaa juani kutwa nzima au hadi siku mbili, wanaweka kwenye mashine baada ya muda mfupi wanawatoa na kuwaingiza sokoni, nani anasema eti Dkt. Mwinyi anashughulika na miradi mikubwa na sio maisha ya watu?” Alihoji Mbeto.
Soma: Tanzania ya kwanza kilimo cha mwani Afrika
Augosti 2024, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ambae kwa sasa ni mgombea wa nafasi ya kiti cha Urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) alisema Serikali yake inakusudia kuweka mkazo zaidi kwenye sekta ya mwani ili kuzalisha bidhaa zenye ubora na kuzipatia soko la uhakika.
Dk. Mwinyi alisema hayo Agosti 21, 2024, Ikulu Zanzibar wakati akizungumza na Balozi wa Umoja wa Ulaya Tanzania Christine Grau.
Alisema asilimia 99 ya wakulima wa zao la mwani Zanzibar ni wanawake, hivyo amemueleza balozi huyo kuangalia haja ya kuwaunga mkono wanawake na wakulima wa mwani nchini, hasa kwa mafunzo na vifaa vya kisasa ili wazalishe mwani wenye ubora utakaoendana sambamba na soko la uhakika.
Mbali na mambo mengine ya maendeleo na uwekezaji ikiwemo utalii, Rais Dk. Mwinyi pia amemueleza Balozi Grau kuwa Uchumi wa Buluu ni sera kuu ya uchumi wa Zanzibar, hivyo alimueleza kuangalia fursa zinazotokana na sera hiyo.
Kwa upande wake, Balozi Christine Grau alisifu juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Rais Dk. Mwinyi na kueleza kuwa wanafanya kazi kwenye maeneo mbalimbali, ikiwemo kushirikiana na jamii kwenye masuala mbalimbali ya maendeleo na ustawi wa jamii Unguja na Pemba.
Katika kuendelea kuinua wakulima wa mwani visiwani humo, Desemba 2023, Rais wa Benki ya Dunia (WB) Ajay Banga Banga, alizungumza na baadhi ya wanufaika wa Mradi wa kilimo cha mwani unaowanufaisha zaidi ya watu 15,000, ambapo asilimia 74 ni wanawake.
Akiwa na waziri wa Fedha wa Tanzania Mwigulu Nchemba, walitembelea mradi huo katika kijiji cha Muungoni, Mkoa wa Kusini, Wilaya ya Kusini, Zanzibar, ambao umewezeshwa na Benki ya Dunia kupitia mfuko wa IDA, kwa ajili ya kukuza uzalishaji wa mwani pamoja na kupanua wigo wa upatikanaji wa soko.
Kiongozi huyo wa WB aliwahakikishia wakulima hao utayari wa Benki hiyo kusaidia juhudi za Serikali za kuboresha maisha ya wakazi wa Zanzibar kupitia program mbalimbali wanazofadhili.
Baadhi ya wanufaika wa mradi huo walieleza kuwa programu hiyo imesaidia kwa kiwango kikubwa kuongeza uzalishaji wa mwani, pamoja na kupunguza gharama na kuboresha maisha yao.
Ziara katika mradi huo ilikuwa ni mwendelezo wa matukio kando ya Mkutano wa Kimataifa wa Tathmini ya Muda wa Kati wa Mzunguko wa 20 wa Benki ya Dunia (IDA20 Mid-Term Review) unaohusisha wakopaji, nchi Wahisani na Menejimenti ya Benki ya Dunia.