Kustaafu ni mabadiliko makubwa na ni sehemu ya maisha anayopitia kila mwajiriwa katika taasisi ama kampuni au sehemu yoyote mtu anayopata fursa ya kufanya kazi.
Watu wengi wanapostaafu hushindwa kuwa na udhibiti wa kifedha na wengi hujikuta wakishindwa kuhimili gharama za maisha baada ya kustaafu.
Ili kuweza kuwa na uchumi imara wakati unapostaafu ni vizuri kujipanga mapema kabla ya muda huo kufika.
Haya ni baadhi ya mambo ya kuzingatia katika kujiweka sawa kiuchumi kuelekea muda wa kustaafu:
Tengeneza bajeti inayotekelezeka
Fuatilia mapato yako na matumizi kama vile (pensheni, uwekezaji, n.k.). hii itakusaidia kujua ni kiasi gani unaingiza na kutumia kiasi gani hivyo kuweza kupanga bajeti yako kulingana na mapato yako.
Weka kipaumbele mahitaji muhimu kama vile mahitaji ya nyumbani ambayo ni lazima, kama chakula, gharama za matibabu, na punguza gharama zisizo za lazima.
Tumia akiba uliyojiwekea kwa uangalifu
Watu wengi wanapostaafu huwa na akiba kubwa, wakati huo wengi huwa wamepokea mafao na fedha mbalimbali baada ya kustaafu. Hapa asilimia kubwa ya watu hujikuta wakitumia fedha zile hovyo wakiona kuwa na nyingi na kusahau kuweka akiba. Wakati mwingine hata kutumia akiba waliyojiwekea wakisahau kwamba kutumia fedha bila kuzalisha hupelekea akiba yote kumalizika. Unashauriwa kutumia akiba yako kwa uangalifu ili kufanya uchumi wako kuwa imara wakati wote baada ya kustaafu ili kuepuka kumaliza fedha zako zote kabla ya wakati na kuwa tegemezi.
Hapa pia unaweza kuwa na mshauri wa masuala ya fedha ambae atakushauri vema masuala hayo.
Punguza madeni na kupunguza mahitaji ikiwa inawezekana
Kama una madeni, lipa madeni yenye riba kubwa kwanza. Punguza matumizi makubwa kadri iwezekanavyo. Kama ulipanga hususani maeneo ya mjini wakati wa ajira, hapa unaweza kuhamia eneo jingine njee ya mji ili kupunguza gharama za pango kwani maeneo mengi ya mjini kodi za pango huwa juu zaidi ya nje ya mji.
Zingatia uwekezaji
Unapostaafu ni vema kuwa na vyanzo vingine vya kujipatia kipato. Hapa unaweza kuwekeza katika sekta mbalimbali ambazo ni za uhakika. Unaweza kununua hisa katika kampuni au biashara nyingine ya uhakika. Epuka uwekezaji usio wa uhakika.
Punguza gharama za afya
Ili kupunguza gharama za matibabu, ni vema kujiandikisha katika Mifumo rasmi ya bima ya Afya kwa ajili ya kupata matibabu. Kuwa na bima ya afya kunatoa nafuu katika matibabu ukizingatia kuwa umri wa kustaafu ni miaka 60 na kuendelea ambapo katika umri huo watu wengi hunyemelewa na magonjwa mbalimbali ya uzeeni.
Epuka udanganyifu wa kifedha
Kuwa mwangalifu kwa miradi ya uwekezaji.
Kamwe usimshirikishe mtu usiyemwamini taarifa zako binafsi hususani za masuala ya fedha zako. Pia ni vema kuzingatia taasisi zinazoaminika katika utunzaji na uwekezaji wa fedha zako.
Fanya uwekezaji tofauti tofauti kulingana na soko
Usiwekeze katika biashara moja kwa muda mrefu, labda kama inakupatia faida kubwa na kipato cha uhakika. Unaweza pia kuwekeza katika maeneo mengine kulingana na soko la uwekezaji linavyokwenda kulingana na majira na mfumuko wa bei.
Tafuta kazi za ziada kama una nguvu
Ndio, kama bado una nguvu ya kufanya kazi unaweza kutafuta kazi hata ya kufanya kwa saa chache, kama wewe ni mwalimu unaweza kuwa unafundisha jioni (Tution) ama kazi yoyote kulingana na taaluma yako. Unaweza kuwa hata mshauri, mwandishi, hizi ni baadhi ya kazi ambazo hazitatumia muda wako mwingi. Mbali na kujiingizia kipato, hii itakusaidia kuweka akili na mwili wako vizuri. Watu wengi hupoteza muelekeo baada ya kustaafu kutokana na kukaa nyumbani bila kujishughulisha. Hii hupelekea kufilisika kifedha na kiakili.
Unashauriwa kujiandaa kwa ajili ya kustaafu kwa kupanga mikakati dhabiti hususani ya kiuchumi kabla ya muda wa kustaafu. Fanya uwekezaji wa kutosha pindi unapokuwa katika ajira ili unapostaafu uwe umejiandaa vema.
Kwa kufuata mbinu hizi, wastaafu wanaweza kufurahia utulivu wa kifedha wakati wakifurahia miaka yao ya starehe. Kustaafu sio mateso, jipange mapema kuelekea wakati wa kustaafu.
Wakati ni sasa, anza sasa.