Home VIWANDANISHATI Wachoma nyama nao watumia nishati safi ya kupikia 2025

Wachoma nyama nao watumia nishati safi ya kupikia 2025

0 comments 211 views

Wachoma nyama nao watumia nishati Agizo la Naibu Waziri Mkuu

Dkt. Doto Biteko kwa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuhakikisha kuwa minada yote nchini inakuwa na miundombinu itakayowawezesha wachoma nyama, mama lishe na baba lishe kutumia nishati Safi ya Kupikia limeanza kutekelezwa ikiwa ni utekelezaji wa ajenda ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha wananchi wote wanatumia Nishati iliyosafi ya kupikia.

Safari ya kuhakikisha minada yote nchini inatumia nishati safi ya kupikia, imeanzia katika mnada wa Msalato jijini Dodoma ambapo Agosti 21, 2025, Dkt. Biteko amegawa majiko banifu kwa mama lishe takriban 27 wanaohudumu katika mnada huo pamoja na majiko ya kuchomea nyama.

Wachoma nyama nao watumia nishati safi ya kupikia - pesatu.com

Naibu Waziri na Waziri wa Nishati Dkt. Dotto Biteko akigawa jiko kwa mmoja wa mama lishe jijini Dodoma.

“Kama mnavyofahamu, Rais alitoa maelekezo kuwa watanzania asilimia 80 ifikapo 2034 watumie nishati safi ya kupikia, maelekezo yake yanaendelea kutekelezwa, tulianza na taasisi zinazolisha watu zaidi ya 100 kuondoa matumizi ya kuni na mkaa ikiwemo magereza yote nchini, shule za Sekondari , vyuo na taasisi nyinginezo lakini moja ya maeneo yaliyobaki ni pamoja na minada ambayo inahudumia watu wengi,” amesema Dkt.Biteko.

Dkt. Biteko ameeleza kuwa kazi ya kufunga mifumo ya Nishati Safi ya Kupikia kwenye minada ilianza na utafiti ili kupata hali halisi ya matumizi ya nishati hiyo ambapo katika utafiti huo, asilimia 89.5 ya wachoma nyama wote walisema hawana uelewa kuhusu nishati safi ya kupikia.

Wachoma nyama nao watumia nishati safi ya kupikia - pesatu.com

Utafiti huo pia utafiti huo umeonesha asilimia 26.3 ya wachoma nyama wamewahi kutumia nishati safi ya kupikia na asilimia iliyobaki hawajawahi kutumia.

Hii ikionesha kuwa bado kuna kazi ya kufanya kuelekea kwenye matumizi ya Nishati Safi ya kupikia.

Amesisitiza kuwa, hatua hizo zinazochukuliwa na Serikali katika Nishati Safi ya Kupikia, ni matunda ya Rais, Dkt.Samia Suluhu Hassan ambaye amejipambanua kama kiongozi mwanamke anayejua machungu ya matumizi ya nishati isiyo safi na wakati wote anaelekeza kuwa yeye anachotaka kuona ni watu wengi hawatumii nishati isiyo safi ya kupikia.

Wachoma nyama nao watumia nishati safi ya kupikia - pesatu.com

June, 2025, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko alizindua Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano wa Nishati Safi ya Kupikia, pamoja na Kampeni ya Kitaifa ya Uhamasishaji na Uelimishaji kuhusu Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.

Alisema lengo la mkakati huo ni kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia na hivyo kuwezesha asilimia 80 ya Watanzania kuhamia katika matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ifikapo 2034.

Soma: Asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati safi ya kupikia ifakapo 2034

Akizindua Mkakati huo wa Mawasiliano jijini Dodoma, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko aliagiza kuwa mkakati huo usiishie kukaa kwenye makabati bali utekelezwe katika ngazi zote za Serikali hadi ngazi ya mtaa bila kusahau Sekta binafsi, wadau wa maendeleo pamoja na vyombo vya Habari kuwa mstari wa mbele katika kuutekeleza.

Katika uzinduzi huo, Dkt. Biteko alimpongeza Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kinara namba moja wa matumizi ya Nishati safi ya kupikia ndani na nje ya nchi ambapo tangu azindue Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati safi ya kupikia (2024-2034) mnamo Mei 08, 2024 matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia nchini yameongezeka kutoka asilimia 6 hadi 16.

Soma zaidi: Matumizi Nishati Safi ya Kupikia yaongezeka kutoka 6% mpaka 16%

“Katika kuthibitisha jinsi anavyolipa umuhimu suala hili la Nishati Safi ya Kupikia, Rais pia ameunda Kitengo cha Nishati Safi ya Kupikia ambacho kina jukumu maalumu la kusimamia ajenda ya nishati safi ya kupikia na kwa kupitia kitengo hiki Serikali itaendelea na shughuli mbalimbali ikiwemo kubuni na kusimamia miradi, pia kusimamia kampeni zote za Kitaifa za uelimishaji na uhamasishaji wa nishati safi ya kupikia,” amesema Dkt. Biteko.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ndie kinara wa ajenda ya nishati safi ya kupikia nchini na Afrika na bado anaendelea kuipeleka ajenda hiyo Kimataifa ili kuhakikisha watu wanapika katika mazingira salama kiafya na kimazingira.

Soma: Nchi za Afrika zapewa wito matumizi nishati safi ya kupikia

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter

Subscribe my Newsletter for new blog posts, tips & new photos. Let's stay updated!