Watumiaji wa vyombo vya moto nchini wanaendelea kufurahia kushuka kwa bei za petroli na dizeli kwa mwezi wa tano mfululizo.
Hata hivyo, watumiaji wa mafuta ya taa wanabaki na hasara kwa sababu bei yake imepanda.
Kushuka na kupanda kwa bei hizo kumetangazwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) kuanzia Jumatano Septemba 03, 2025.
Taarifa iliyosainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Ewura James Mwainyekule inaeleza kuwa bei za petroli na dizeli zimeshuka kwa Shilingi 36 na 23 mtawalia, kwa mafuta yanayopita Bandari ya Dar es Salaam, Tanga na Mtwara.
“Bei za mafuta hapa nchini zinazingatia gharama za mafuta yaliyosafishwa (FOB) katika soko la Uarabuni. Katika bei kikomokwa Septemba 2025, bei za mafuta katika soko la dunia zimepungua kwa asilimia 0.2 kwa mafuta ya petrol na kwa asilimia 5.5 kwa dizeli na mafuta ya taa kwa asilimia 3.5.
Kwa mwezi Septemba 2025, gharama za kuagiza mafuta (premiums) katika Bandari ya Dar es Salaam zimeongezeka kwa wastani wa asilimia 20.73 kwa mafuta ya petrol, asilimia 7.75 kwa mafuta ya dizeli na asilimia 2.62 kwa mafuta ya taa,” imeeleza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa kwa upande wa Bandari ya Mtwara hakuna mabadiliko.
Bandari ya Tanga bei zimepungua kwa aisilimia 12.66 kwa mafuta ya petrol na dizeli asilimia 12.66.

Kwa Bandari ya Dar es Salaam:
Petroli: Sh2,807 (ilikua Sh2,843)
Dizeli: Sh2,754 (ilikua Sh2,777)
Mafuta ya Taa: Sh2,774 (imepanda kutoka Sh2,768)
Kwa Bandari ya Tanga:
Petroli: Sh2,868 (ilikua Sh2,904)
Dizeli: Sh2,816 (ilikua Sh2,839)
Mafuta ya Taa: Sh2,835 (imepanda kutoka Sh2,829)

Kwa Bandari ya Mtwara:
Petroli: Sh2,899 (ilikua Sh2,935)
Dizeli: Sh2,847 (imeshuka kutoka Sh3,020)
Mafuta ya Taa: Sh2,866 (imepanda kutoka Sh2,860)
Ewura inaeleza kuwa gharama za mafuta (FOB) na gharama za uagizaji (premiums) zinalipiwa kwa kutumia fedha za kigeni ikiwemo Dola ya Marekani. Kwa bei za mwezi Septemba 2025, wastani wa gharama za kubadilisha fedha za kigeni (Applicable Exchange Rate) umepungua kwa asilimia 3.96.

Ewura pia imewataka wauzaji wa mafuta kuandika bei zao kwenye mabango makubwa na wazi yakionesha bei za mafuta, punguzo na vivutio vya kibiashara vinavyotolewa na kituo husika.
“Pale ambapo inawezekana kuchagua, wateja wanashauriwa wanunue bidhaa za mafuta katika vituo vya mafuta kwa bei nafuu Zaidi ili kushamirisha ushindani.
Ni kosa kuuza mafuta bila kuweka mabango ya bei yanayoonekana vizuri kwa wateja. Adhabu kali itatolewa kwa kituo husika kwa kutotekelezwa matwakwa ya kisheria kwa mujibu wa kanuni husika,” imeonya taarifa hiyo.
Ewura imewataka wauzaji wa bidhaa hizo kuhakikisha wanatoa stakabadhi (risiti) za kielektroniki (kutoka kwenye mashine za Electronic Fiscal Pump Printers EFPP) na wanunuzi wahakikishe wanapata stakabadhi hizo za malipo zikionesha jina la kituo, tarehe, aina ya mafuta yaliyonunuliwa na bei kwa lita.
Ewura inaeleza kuwa stakabadhi hizo zitatumika kama kidhibiti kwa wanunuzi wa mafuta endapo kutajitokeza malalamiko au kuuziwa mafuta yasiyo na kiwango cha ubora unaotakiwa.
“Stakabadhi hizo pia zitasaidia kurahisisha ukusanyaji wa kodi za serikalii zitokanazo na mauzo ya bidhaa za mafuta,” imesema taarifa hiyo.
Soma: Bei ya mafuta yaongezeka mwezi Februari
