Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo, ameongoza kikao cha wataalam kutoka taasisi mbalimbali za Serikali kwa ajili ya kujadili mikakati ya kudhibiti utoroshaji wa madini nchini.
Kikao hicho kimefanyika Oktoba 07, 2025, katika Ukumbi wa Mikutano wa Wizara ya Madini Mtumba jijini Dodoma.
Akizungumza katika kikao hicho, Mbibo amesema kuwa ni wajibu wa kila Mtanzania kushiriki kikamilifu katika kulinda rasilimali za taifa, hasa madini, kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
“Utoroshaji wa madini ni tishio kwa uchumi na usalama wa taifa letu. Tunapaswa kushirikiana kwa dhati katika kudhibiti mianya yote inayochangia vitendo hivi,” amesema Mbibo.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo.
Aidha, amesema kuwa utoroshaji wa madini umekuwa ukiliingizia taifa hasara kubwa ya mapato, na kwamba ipo haja ya dharura ya kuunganisha nguvu za pamoja katika kudhibiti vitendo hivyo haramu.
“Madini ni miongoni mwa rasilimali muhimu zinazotegemewa katika kuchochea maendeleo ya taifa letu. Hatuwezi kukubali kuendelea kupoteza mapato kwa sababu ya mianya ya utoroshaji. Ni wajibu wa kila mmoja wetu kama watanzania wazalendo kushiriki katika vita hii,” amesema Mbibo.
Katika kikao hicho, Mbibo ameeleza kuwa Serikali inahitaji kuwa na mfumo thabiti na shirikishi wa udhibiti wa madini kuanzia migodini, kwenye vituo vya ukaguzi, hadi viwanja vya ndege, bandari na mipaka yote ya nchi.
Pia, ametoa wito wa kuundwa kwa timu maalum za kitaifa zenye wataalam kutoka taasisi mbalimbali, zitakazoshirikiana katika kufanya uchunguzi, ufuatiliaji na ulinzi wa madini, hasa katika maeneo ambayo yameonekana kuwa na mianya mikubwa ya utoroshaji.
“Tunapaswa kuwekeza katika vifaa vya kisasa vya kuchunguza na kubaini madini hususan madini ya vito kwa haraka na kwa uhakika. Vifaa hivi vitasaidia sana kuzuia mbinu mpya zinazotumiwa na wanaojihusisha na utoroshaji,” amesisitiza.
Mbibo pia amependekeza kuanzishwa kwa mpango wa mafunzo endelevu kwa wataalam wanaofanya kazi katika maeneo ya ukaguzi ili kuwajengea uwezo wa kutambua aina mbalimbali za madini, mbinu za usafirishaji.
Soma: Tsh Bilioni 14.3 kutumika ujenzi wa maabara ya kuchunguza madini
Amependekeza kuanzishwa kwa mpango wa mafunzo endelevu kwa wataalam wanaofanya kazi katika maeneo ya ukaguzi ili kuwajengea uwezo wa kutambua aina mbalimbali za madini, mbinu za usafirishaji haramu na matumizi ya teknolojia ya kisasa katika kudhibiti biashara hiyo haramu.
Katika hitimisho la kikao, wadau walikubaliana kuweka mikakati ya haraka ya utekelezaji wa maazimio yaliyopitishwa, ikiwa ni pamoja na kuandaa mpango kazi wa pamoja utakaohakikisha udhibiti wa utoroshaji wa madini unafanyika kwa ufanisi na kwa muda mrefu.
Kikao hicho kimehusisha ushiriki wa taasisi mbalimbali za Serikali ikiwemo Wizara ya Madini, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Tume ya Madini, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), pamoja na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA).
Soma Zaidi: Tanzania kununua helikopta kuchunguza madini ardhini
Katika tukio lingine, kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa mwaka 2025 Ismail Ussi amezindua Kiwanda cha Kuchenjua Madini ya Dhahabu Wilayani Chunya cha Kampuni ya Ken Gold kilichogharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 2.
Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika Oktoba 7, 2025, Ussi amesema Mbeya ni Mkoa unaendelea kufanya vizuri katika Sekta ya Madini hususan Wilaya ya Chunya kutokana na shughuli za madini na kuongeza kwamba, Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa wawekezaji wazawa na wageni.
Ameeleza kuwa, moja ya masuala ambayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa akiyapa msukumo ni Sekta ya Madini na hususan ushiriki wa wazawa kwenye uchumi wa madini.
“Mhe. Mkuu wa Wilaya tuwape ushirikiano wa kutosha wawekezaji wetu wakiwemo wazawa. Mfano mwekezaji huyu mzawa angeweza kwenda kuwekeza mkoa mwingine wenye madini lakini amechagua Chunya. Mwenge wa Uhuru umewaka Sekta ya Madini na kutoa heshima,” amesema Ussi.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Chunya Mbarak Alhaji Batenga amesema hadi sasa Wilaya hiyo ina jumla ya mitambo ya kuchenjua dhahabu ipatayo 45 na kwamba ni mkoa wa pili wa kimadini kwa uzalishaji wa dhahabu baada ya Geita.
” Ndugu Kiongozi wa Mwenge, Dkt. Samia Suluhu ametupa maelekezo ya kulinda rasilimali zetu, na nikueleze tu Chunya ni Wilaya isiyovuma kwenye madini lakini ipo. Sisi ni wa pili kwa uzalishaji wa dhahabu nyuma ya Geita,’’ amesema Batenga.
Ameongeza kwamba, shughuli za uchimbaji madini zinaendelea kuchangia maendeleo na kutolea mfano wa uchimbaji mdogo kwamba hivi sasa mchango wa wachimbaji wadogo kwenye maduhuli ya Serikali umefikia asilimia 40.