Home FEDHA Wataalam wa kusimamia Bajeti ya Serikali wameagizwa kutumia mafunzo ya Mfumo ulioboreshwa

Wataalam wa kusimamia Bajeti ya Serikali wameagizwa kutumia mafunzo ya Mfumo ulioboreshwa

0 comments 131 views

Wataalam wa wanaoandaa na kusimamia Bajeti ya Serikali wameagizwa kutumia mafunzo ya Mfumo ulioboreshwa wa Uandaaji na Usimamizi wa Bajeti (CBMS), kuboresha utendaji kazi katika usimamizi wa uandaaji na utekelezaji wa Bajeti ya Serikali.

Agizo hilo limetolewa jijini Dodoma na Kamshina wa Bajeti, Wizara ya Fedha, Meshack Anyingisye wakati akifungua mafunzo ya Mfumo wa CBMS ulioboreshwa na baadae kufanya Tathmini ya Utekelezaji wa Bajeti ya Serikali ya Mwaka 2024/25, Maandalizi ya Bajeti ya Serikali ya Mwaka 2025/26 na kupata maoni ya kuboresha mchakato wa maandalizi ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2026/27.

Anyingisye alisema wataalam hao ni watu muhimu sana katika uandaaji na utekelezaji wa bajeti ya Serikali hivyo watumie mafunzo hayo kusimamia bajeti na kushauri Idara tumizi namna bora ya kutekeleza bajeti zao pamoja na kuboresha usimamzi wa bajeti ya Serikali.

“Usimamizi wa bajeti sio jukumu la Wizara ya Fedha tu, ni jukumu la kila mmoja wetu hivyo ni vema tukatekeleza majukumu yetu kikamilifu katika kushauri na kuchakata takwimu mbalimbali kutoka katika bajeti zetu”, alisisitiza Anyingisye.

Aidha, alisisitiza kuwa ushiriki wa watumishi hao katika kikao hicho unaashiria kujitolea kwa pamoja katika kuboresha utekelezaji na usimamizi wa bajeti ya Serikali, kuongeza ufanisi katika mchakato wa bajeti na kuhakikisha vipaumbele vya Serikali vinatekelezwa ipasavyo.

Awali akizungumzia mafunzo hayo, Kamishna Msaidizi wa Bajeti anayeshughulikia uchambuzi na mbinu za kibajeti Wizara ya Fedha, Fundi Makama, alisema mafunzo hayo yamehusisha wadau kutoka Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Ofisi za Wakuu wa Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Alisema mafunzo hayo ya siku tano (5) yatatolewa kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza itahusu mafunzo ya Mfumo wa Uandaaji na Usimamizi wa Bajeti (CBMS) ulioboreshwa na awamu ya pili itajikita kwenye Tathmini ya Uandaaji wa Bajeti ya 2025/26 na tathmini ya utekelezaji wa Bajeti ya 2024/25.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter

Subscribe my Newsletter for new blog posts, tips & new photos. Let's stay updated!