Nchi za Tanzania na Kenya zinatarajia kufanya mazungumzo juu ya katazo la biashara ndogo ndogo lililowekwa na Tanzania kwa wafanyabiashara wa kigeni.
Katibu wa Baraza la Mawaziri, Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Beatrice Askul aliiambia Kamati ya Bunge ya Ulinzi, Ujasusi na Mambo ya Nje Bunge kuwa kikosi cha wataalamu kipo Tanzania kujadiliana kuhusu kuondolewa kwa katazo hilo.

Katibu wa Baraza la Mawaziri, Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Beatrice Askul
Askul alisema Tanzania imeahidi Kenya kuwa marufuku hayo hayathiri raia wake na masuala yoyote yatatatuliwa kwa njia ya kidiplomasia.
Askul alisema: “ingawa katazo hilo linatokana na Sheria ya Tanzania, haiwezi kuwekwa moja kwa moja kwa Kenya. Ninafikiri wametuambia marufuku hiyo sio kwa Kenya. Walikuwa wakilenga maslahi yao mengine katika jambo hili. Na wametuhakikishia kuwa kupitia ubalozi wetu, ikiwa raia yeyote wa Kenya atakumbwa na hili, wataweza kushughulikia.
“Na hili ni jambo la ndani. Tatizo lao lilikuwa China na Wachina ambao walikuwa wakiingilia masoko yao. Wachina na Waturuki, ambao sasa wamo katika biashara zote ambapo huenda huko Kenya ni vivyo hivyo. Hilo ndilo tatizo lao.”
Alisema kuwa wajasiriamali wadogo na wakati (MSMEs) biashara zao zimeingiliwa na wafanyabiashara wa kigeni.
“Kwa hivyo, mambo hayo ndiyo Tanzania inataka kuyashughulikia kwa mujibu wa sharia.
Na wametuhakikishia kuwa ikiwa Mkenya yeyote atakumbana na hilo, anapaswa kuwasilisha kwa mamlaka husika.
Hawakuwa na njia nyingine ya kuwasilisha habari isipokuwa kusema ‘wageni’. Kwa hivyo, sisi tumeingia katika kundi hilo. Lakini kama nilivyosema, katika utekelezaji, walishirikiana nasi na tunaamini kuwa wana tatizo kubwa ambalo wanataka kulishughulikia,” amesema Askul.
“Tuna timu ya wataalamu wanaojadiliana sasa hivi nchini Tanzania. Tutakutana kama Mawaziri Oktoba 03, 2025 nchini Tanzania ambapo tunatarajia kusaini makubaliano ya pande zote mbili.”
Mnamo Julai, Tanzania ilitoa tangazo la kisheria likikataza wageni kufanya biashara 15 tofauti.
Kenya ilisema haitafanya kisasi dhidi ya uamuzi wa Tanzania wa kukataza wageni, lakini iliahidi kujadili kwa njia ya kidiplomasia ili kutatua suala hilo ambalo serikali yake ilisema raia wake wanaweza kupoteza hadi SH milioni 19 ikiwa vikwazo vitadumu.
Mnamo Agosti 2025, Waziri Mkuu wa Baraza la Mawaziri, Musalia Mudavadi, aliliambia Bunge kuwa Kenya haiwezi kupingana na majirani zake katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ikizingatiwa kwamba nchi hiyo ndiyo inayofaidika zaidi na biashara katika ukanda huo.

Waziri Mkuu wa Baraza la Mawaziri, Musalia Mudavadi.
Mudavadi, aliita vikwazo hivyo vya biashara kuwa vinakiukia ahadi za Tanzania juu ya ukombozi wa biashara ya huduma chini ya Itifaki ya Soko la Pamoja la EAC.
Mudavadi alisema soko la EAC ni muhimu sana kwa Kenya, likiwakilisha asilimia 64 ya Biashara Afrika.
“EAC ni kundi muhimu kwetu na hatuwezi kuanza kugombana na majirani zetu. Kama kuna masuala, lazima tuyatatue kidiplomasia.
Hatutaki kufika kwenye kiwango cha kulipiza kisasi. Thamani ya kikundi hiki cha kiuchumi ni muhimu sana kwetu,” alisema Mudavadi.
Mnamo Julai 28, 2025, Tanzania ilitoa Leseni ya Biashara (Kukatazwa kwa Shughuli za Biashara kwa Wasiokuwa Raia) ya 2025, kulingana na Sheria ya Leseni za Biashara (Sura ya 101) ya Sheria za Tanzania.
Amri hiyo ilikataza rasmi watu wasio raia wa Tanzania kufanya biashara 15 zilizoainishwa ikilenga kuwezesha uchumi wa raia wa Tanzania pamoja na kulinda soko la ndani.
Sheria hiyo inakata wasiokuwa raia kushiriki katika shughuli maalum 14 za biashara nchini Tanzania. Shughuli hizi ni pamoja na uuzaji wa bidhaa kwa jumla na rejareja (isipokuwa maduka makubwa, duka maalum la bidhaa, na vituo vya jumla kwa wazalishaji wa ndani), wakala wa fedha kwa njia ya simu (mobile money), ukarabati wa simu za mkononi na vifaa vya elektroniki, biashara ya saluni (salon) (isipokuwa ikiwa inafanyika katika hoteli au kwa ajili ya utalii).
Nyingine ni wageni kuendesha au kumiliki:
Huduma za usafi wa nyumbani, ofisini na mazingira, uchimbaji mdogo wa madini, huduma za posta na usafirishaji wa vifurushi, kuongoza watalii ndani ya nchi (tour guiding), uendeshaji wa vituo vya redio/runinga (TV), uendeshaji wa makumbusho au maduka ya vitu vya kihistoria (curio shops).
Huduma za wakala/mkandarasi (brokerage) au wakala wa mali isiyohamishika (real estate), huduma za kusafirisha na kusaidia malipo ya forodha (clearing and forwarding), ununuzi wa mazao shambani (on-farm crop purchasing), umiliki/uendeshaji wa mashine za kamari (kwenye maeneo yasiyo ya kasino) na umiliki na uendeshaji wa viwanda vidogo vidogo (micro and small industries).
Katazo hilo linaanza kutekelezwa mara moja mara baada ya kuchapishwa tarehe 28 Julai 2025, huku kipindi cha mpito kikiwemo kwa wale waliokuwa tayari wakimiliki leseni, na inajumuisha adhabu kubwa kwa watakaokiuka.
Mamlaka za Leseni za raia wa Tanzania zilipigwa marufuku kutoa au kuhuisha leseni kwa wasio-raia katika sekta hizi maalum, huku wakiukaji wakikabiliwa na faini ya takribani Shilingi milioni 10 za Kitanzania na kufutiwa visa au vibali vya makazi.
Soma: Tanzania yapiga marufuku mazao ya Afrika Kusini, Malawi