Home VIWANDAUZALISHAJI Wageni wafurika kuionja, kununua Misitu Honey ya TFS

Wageni wafurika kuionja, kununua Misitu Honey ya TFS

0 comments 201 views

Misitu Honey, asali inayozalishwa na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) imekuwa kivutio kwa wageni wa ndani nan je ya nchi Katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) (DITF) yanayoendelea jijini Dar es Salaam.

Watu wengi wanaotembelea banda la TFS wameonekana wakivutiwa na asali hiyo ambapo wengi huionja na kuinunua.

Wakazi na wageni kutoka mataifa mbalimbali wamefurika kwenye duka la TFS lililopo ndani ya Banda la Wizara ya Maliasili na Utalii, wakijionea na kuonja bure ladha halisi ya asali safi inayozalishwa kutoka misitu inayosimamiwa kwa uangalizi mkubwa.

Mhifadhi Subira Matumbwa, amesema kuwa idadi kubwa ya watu wamevutiwa na ladha safi, rangi halisi na ubora wa Misitu Honey unaotokana na mnyororo wa uzalishaji wa kitaalamu na uhifadhi endelevu wa misitu.

“Watu wengi wamefurahia kuonja bure na kununua. Wengi wanapongeza ladha safi isiyo na kemikali, na sifa nyingine kubwa ni kuwa asali hii ina virutubisho vya asili vinavyosaidia kuongeza kinga ya mwili, kuimarisha afya na haina viambato bandia,” amesema Mhifadhi Matumbwa.

Wageni wafurika kuionja na kununua asali ya Tanzania maonesho ya Sabasaba

Mgeni akionja asali ya Tanzania katika Maonesho ya Biashara jijini Dar es Salaam (Sabasaba)

Mbali na asali safi, banda hilo pia limepamba maonesho kwa bidhaa za asali zilizoongezewa thamani kama asali yenye mchanganyiko wa ndizi, mdalasini na hata alizeti, huku asali ya alimondi ikiwa kivutio kipya kabisa. Bidhaa hizo zinapatikana kwa ujazo unaokidhi mahitaji ya kila mteja kuanzia gramu 500 hadi kilo 5.

Wananchi wametakiwa kutumia fursa hii kufika Sabasaba, kutembelea banda la TFS na kujipatia asali bora ya Misitu Honey kwa manufaa ya afya zao na kuongeza kipato kwa kuchangia sekta ya misitu endelevu.

Akitoa wito kwa wananchi Mhifadhi Matumbwa amehimiza kuwa “tunawahamasisha Watanzania wajitokeze kwa wingi Sabasaba. Waje waonjee bure, wanunue na waendelee kutumia Misitu Honey — asali bora, salama na yenye manufaa kwa afya zao na familia zao.”

Wageni wafurika kuionja na kununua asali ya Tanzania maonesho ya SabasabaMbali na hayo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi na Meneja wa TEHAMA na Takwimu wa TFS, Harold Chipanha amepongeza hatua kubwa za kidigitali zinazotekelezwa na TFS katika maonesho hayo.

Chipanha alitembelea banda la TFS na kujionea namna wakala huo umefanikiwa kutumia mifumo ya TEHAMA kuboresha huduma kwa wananchi na wadau wa sekta ya misitu, ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Serikali ya Awamu ya Sita kuhakikisha taasisi zote za umma zinatumia teknolojia kurahisisha upatikanaji wa huduma.

Akizungumza baada ya kupata maelezo ya kina kutoka kwa maafisa wa TFS, Chipanha alisema mfumo wa satelite unaotumika kufuatilia moto misituni umeleta mapinduzi makubwa kwa sababu unarahisisha upatikanaji wa taarifa sahihi na kwa wakati, hivyo kusaidia taasisi nyingi zinazohitaji taarifa hizo katika kulinda na kuhifadhi misitu.

“Mfumo huu umewezesha TFS kutoa taarifa kwa wakati sahihi (ontime) na kwa usahihi. Ni jambo kubwa na la kupongezwa kwa sababu linasaidia katika kuzuia uharibifu wa misitu unaotokana na moto,” alisema Chipanha.

Aidha, Chipanha alitembelea pia banda la Utalii Ikolojia na kushuhudia namna programu ya kidigitali ya e-Misitu inavyofanya kazi kwa kuwawezesha wananchi kubook safari za kutembelea vivutio vya misitu kwa njia rahisi kupitia simu zao za mkononi. Alisema kuwa mfumo huo ni kielelezo cha jinsi TFS inavyotekeleza dhamira ya Serikali ya kutoa huduma bora kidigitali.

Mbali na mifumo ya moto na utalii, Chipanha alifurahishwa pia na ubunifu wa TFS katika uzalishaji na uuzaji wa asali ya Misitu Honey ambayo inauzwa kupitia mfumo wa kielektroniki wa Serikali (Government e-Payment Gateway).

Akipata maelezo kwenye banda hilo Chipanha alishuhudia mfumo wa Honey Traceability System unaotumika kufuatilia ubora wa asali kuanzia kwa mfugaji hadi inapofika sokoni.

Nae Mwenyekiti wa Banda la Maonesho ambaye pia ni Mkurugenzi wa Masoko wa Bodi ya Utalii Tanzania, Ernest Mwamaja, alisema TFS imevuka matarajio kwa kuboresha muonekano wa mabanda, bidhaa na elimu inayotolewa sambamba na ushirikiano na wadau wa uhifadhi.

“Itoshe kusema TFS mwaka huu wamefanya mapinduzi makubwa. Sijawahi kuona jambo kubwa kama hili, nawapongeza sana kwa ubunifu na maandalizi haya ya kiwango cha juu,” alisema Mwamaja mbele ya Kamishna wa Uhifadhi, Prof. Dos Santos Silayo.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter

Subscribe my Newsletter for new blog posts, tips & new photos. Let's stay updated!