Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Emmanuel Tutuba, ameongoza mjadala maalum wa kitaaluma katika kongamano la uchumi lililofanyika Julai 18, 2025 jijini Lilongwe, Malawi. Kongamano hilo lilikuwa sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwa Benki Kuu ya Malawi, ambapo mgeni rasmi alikuwa Rais wa Jamhuri ya Malawi, Dkt. Lazarus Chakwera.

Benki Kuu ziwe washirika mageuzi ya kiuchumi.
Mjadala huo uliobeba mada “Kurudi kwenye Misingi: Je, kuna nafasi kwa Benki Kuu katika nchi zenye kipato cha chini kuingilia kati mfumo wa ugavi?” uliongozwa na Gavana alisisitiza umuhimu wa kutathmini kwa kina nafasi ya benki kuu katika kusaidia ukuaji wa uchumi sambamba na jukumu lake la msingi la kuhakikisha uthabiti wa bei.
Katika hotuba yake ya utangulizi, Gavana alieleza kuwa, licha ya mageuzi yanayoendelea katika utekelezaji wa sera za fedha, kutoka kutumia mfumo unaolenga jumla ya fedha kwa kuzingatia viwango vya ubadilishaji wa fedha hadi kutumia mifumo inayojikita kwenye viwango vya riba, bado nchi nyingi zenye kipato cha chini zinakabiliwa na changamoto kubwa, hususan katika miundombinu ya kutekeleza sera hizo ipasavyo.
“Katika mazingira ambapo mfumuko wa bei unasababishwa zaidi na mishtuko ya upande wa ugavi kama ilivyo kwa nchi nyingi barani Afrika zinazotegemea kilimo ikiwemo Malawi, ni lazima tujiulize kama wigo wa jukumu la Benki Kuu unaweza kupanuliwa ili kushirikiana kikamilifu katika kukuza uzalishaji wa ndani bila kupoteza lengo msingi la uthabiti wa bei”, alisema Gavana Tutuba.
Akihitimisha mjadala huo, Gavana Tutuba alisisitiza kuwa Benki Kuu haziwezi kubaki kama wasimamizi wa sera za uchumi, bali zinapaswa kuwa sehemu ya suluhisho, hasa katika mazingira ambapo changamoto za kiuchumi zinahitaji ushirikiano wa taasisi zote za kiuchumi.
Kongamano hilo limejumuisha magavana wa benki kuu kutoka nchi za SADC, viongozi wa serikali, wataalam wa uchumi, wachambuzi wa sera, na wawakilishi wa mashirika ya kitaifa na kimataifa, kwa lengo la kujadili changamoto na mustakabali wa sera za fedha katika nchi zenye kipato cha chini.
Akiwa nchini Malawi, Gavana Tutuba, alifanya ziara katika Ubalozi wa Tanzania nchini Malawi, uliopo jijini Lilongwe. Katika ziara hiyo, Gavana alipokelewa na Balozi wa Tanzania nchini humo, Mhe. Agnes Kayola.
Akizungumza wakati wa mapokezi hayo, Balozi Kayola alieleza kuwa uhusiano baina ya Tanzania na Malawi unaendelea kuimarika, hususan katika eneo la biashara. Alisisitiza kuwa kiwango cha biashara kati ya nchi hizo mbili kimeongezeka kutokana na juhudi za kukuza diplomasia ya uchumi, ambayo inalenga kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi baina ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Kwa upande wake, Gavana Tutuba alieleza kuwa sekta ya fedha nchini Tanzania inaendelea kuimarika, hali inayochangia kukua kwa uchumi wa nchi. Alibainisha kuwa utekelezaji thabiti ya sera za fedha pamoja na usimamizi mzuri wa uchumi umeifanya Tanzania kuwa sehemu salama na ya kuvutia kwa wawekezaji wa ndani na wa kimataifa.
Aidha, alimtaka Mhe. Balozi Kayola kuendelea kuhamasisha wawekezaji kutoka Malawi na nchi jirani kuja kuwekeza nchini Tanzania, akisisitiza kuwa mifumo ya uwekezaji iliyopo ni rafiki kwa maendeleo ya biashara na viwanda.
Naye Balozi Kayola alieleza kuwa nchini Malawi pia kuna fursa nyingi za uwekezaji, na hivyo kuwahimiza Watanzania kuchangamkia nafasi hizo ili kukuza ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi hizi mbili jirani.
